Jeshi la Polisi Nchini Lapewa Siku 2 Kumtafuta na Kumpata Mwandishi wa Habari Kutoka Zanzibar, Anayedaiwa Kutekwa - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Mar 2016

Jeshi la Polisi Nchini Lapewa Siku 2 Kumtafuta na Kumpata Mwandishi wa Habari Kutoka Zanzibar, Anayedaiwa Kutekwa

Baraza la habari nchini Tanzania MCT kwa kushirikiana na taasisi nyingine nne zimetoa siku mbili kuanzia leo kwa jeshi la polisi nchini kuhakikisha linafanya uchunguzi na kufanikiwa kumpata mwandishi wa habari Bi. Salma Said anayedaiwa kutekwa.

Wakitoa tamko la pamoja, Katibu Mtendaji wa MCT Bw. Kajubi Mukajanga, Mkurugenzi wa mtandao wa watetezi wa haki za binadamu THRDC Bw. Onesmo Olengurumwa pamoja na mwenyekiti wa jukwaa la wahariri TEF Bw. Theophil Makunga wamesema kitendo hicho kinakwenda kinyume na misingi ya haki za binadamu.

Viongozi hao wamesema kuwa Licha ya kitendo hicho pia kuminya uhuru wa wanahabari na haki ya kupata habari, lakini pia kinajenga hofu kubwa miongoni mwa wanahabari na jamii kwa ujumla.
Aidha vyombo hivyo vimetaka vyombo vya usalama kuhakikisha vitisho vyote dhidi ya wanahabari na watetezi wa haki za binadamu visiwani Zanzibar vinakomeshwa na kuwaacha wawe huru kufanya kazi zao katika kipindi cha uchaguzi wa marudio.

Hivi karibuni Bi. Salma amekuwa akitoa taarifa mbalimbali za hali ya kisiasa visiwani Zanzibar kupitia Idhaa ya Kiswahili ya Ujerumani na mitandao ya kijamii ambapo alisema kuwa kuandika kwake habari hizo alikuwa akipata vitisho kutoka kwa watu wasiojulikana na hapo jana katika uwanja wa ndege wa Julius Nyerere jijini Dar es salaam ilisemekana mwandishi huyo alitekwa na watu wasiojulikana.