Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli leo ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa Kinyerezi namba mbili, uliopo katika wilaya ya Ilala Mkoani Dar es salaam.
Mradi huo utakapokamilika utakuwa na uwezo wa kuzalisha megawatts 240 za umeme.
Mradi huo ambao utazalisha umeme kwa kutumia gesi asilia inayosafirishwa kwa bomba kutoka Mtwara, unatarajiwa kuanza kuzalisha umeme katika kipindi cha kuanzia miezi 21 hadi 28 utakapokamilika kabisa.
Kuanza kwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme huo, kunafuatia juhudi zilizofanywa na serikali ya awamu ya tano ya kufanikisha upatikanaji wa shilingi bilioni 120, ikiwa ni asilimia 15 ya fedha zilizopaswa kutolewa na Tanzania na fedha nyingine shilingi Bilioni 292 zimetolewa na Japan.
Mradi huu umetanguliwa na mradi wa Kinyerezi namba moja ambao una uwezo wa kuzalisha megawatts 150 za umeme, na mitambo yake tayari imeanza uzalishaji wa megawatts 105 zilizoingizwa katika gridi ya Taifa.
Pamoja na kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Kinyerezi namba mbili, Rais Magufuli amekagua mitambo ya kuzalisha umeme ya mradi wa Kinyerezi namba moja, ambapo Mkuu wa Kituo cha Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) cha Kinyerezi Mhandisi John Mageni, ametoa maelezo kuwa shirika hilo lina mpango wa kupanua uzalishaji wa umeme katika mradi huo kutoka megawatts 150 hadi kufikia megawatta 335, kwa kuongeza mitambo ya kufua umeme kwa teknolojia inayojumuisha matumizi ya gesi asilia na mvuke uzalishwao na mitambo hiyo.
Baada ya ya kupokea maelezo hayo, Rais Magufuli ameridhia kuwa serikali yake itatoa dola za kimarekani milioni 20, kwa ajili ya kufanikisha upanuzi wa mradi huo na ameagiza kuwa wataalamu wa TANESCO washirikiane na mkandalasi kuhakikisha upanuzi huo unafanyika haraka iwezekanavyo, badala ya muda wa miezi 12 uliopangwa.
Akizungumza na wananchi waliojitokeza katika sherehe za uzinduzi wa mradi huo, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameiagiza Wizara ya Nishati na Madini na TANESCO, kuanza kuachana na mitambo ya kukodi kwa ajili ya kuzalisha umeme, na badala yake nchi ijenge mitambo yake yenyewe ili kuondokana na gharama kubwa za nishati hiyo muhimu.
"Waziri, ukiona mtaalamu anakuletea mapendekezo ya kutaka kukodi mitambo ya kuzalisha umeme, badala ya kuleta mapendekezo ya kununua mitambo yetu wenyewe ujue mtaalamu huyo hafai, mtoe" Amesisitiza Rais Magufuli.
Ameongeza kuwa tafiti zimethibitisha kuwa hadi sasa Tanzania ina zaidi ya futi za ujazo Trilioni 57 za gesi asilia, ambayo itazalisha umeme wa kutosheleza mahitaji ya ndani, na umeme mwingine kuuzwa nje ya nchi ikiwemo Kenya ambayo tayari imeomba kuuziwa umeme kutoka Tanzania.
Aidha, Rais Magufuli ametoa onyo kwa TANESCO kuwa hatarajii kusikia bwawa la maji la Mtera limeishiwa maji, kwa kuwa katika msimu huu wa mvua maeneo ya Iringa yalikuwa na mvua nyingi ambazo zimesababisha hadi mafuriko mafurukio.
Kwa upande wake, Waziri wa Nishati na Madini Prof. Sospeter Muhongo amesema tangu serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, juhudi zilizofanyika zimefanikisha kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka megawatts 800 hadi kufikia megawatts 1,000 kiasi ambacho ni pungufu kwa megawatts 20 tu, ikilinganishwa na mahitaji ya megawatts 1020 za sasa.
Ameongeza kuwa pamoja na kuweka jiwe la msingi la mradi wa Kinyerezi namba mbili, hivi karibuni serikali inatarajia kujenga miradi mingine ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia, ikiwemo Kinyerezi namba tatu utakaozalisha megawatts 600, Kinyerezi namba nne utakaozalisha megawatts 300, na mingine itakayojengwa Lindi na Mtwara.
Prof. Muhongo amebainisha kuwa mpaka sasa gesi asilia inazalisha kati ya asilimia 50 na 60 ya umeme wote hapa nchini, Maji yanazalisha asilimia 30 hadi 40, na umeme unaozalishwa kwa mafuta hauvuki asilimia 10.
Sherehe hizo zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Balozi wa Japani hapa nchini Mheshimiwa Masaharu Yoshida, Wabunge wa kamati ya Nishati na Madini, wafadhili wakiwemo Benki ya Dunia, Benki ya Afrika na Shirika misaada la Japan (JICA).