Wabunge na madiwani kutoka vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wameandamana hadi ofisi za Jiji wakitaka waambiwe tarehe ya uchaguzi wa umeya wa Dar es Salaam ndani ya siku saba.
Wakiwa kwenye ofisi hizo jana, wawakilishi hao wa wananchi walisema waliamua kwenda kwa njia ya kistaarabu, lakini wasipoambiwa tarehe ya uchaguzi huo watakwenda kwa njia ambayo wanaijua wao.
Akizungumza kwa niaba ya madiwani hao, Mbunge wa Jimbo la Ukonga (Chadema), Waitara Mwita, alisema maandamano yao yalikuwa ya amani kutaka kukutana na Mkurugenzi wa Jiji ili kujua hatma ya uchaguzi huo.
Alisema Jiji linatakiwa kutangangaza tarehe ya uchaguzi huo ndani ya siku saba na endapo hawatafanya hivyo wanachama wa Ukawa watajua cha kufanya.
“Bajeti ya Jiji la Dar es Salaam imepitishwa bila kushirikishwa madiwani wa Ukawa," alisema Waitara ambaye mapema wiki hii alifikishwa mahakamani pamoja na Mbunge wa Kawe, Halima Mdee wakituhumiwa kumpiga msimamizi wa uchaguzi huo, kikao kilipoahirishwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
"Meya wetu tukimpitisha lazima tutaiondoa hiyo bajeti iliyopitishwa bila kuwashirikisha madiwani wetu.”
Aidha, Mwita alisema sheria inatamka kuwa Meya anapaswa kuwa amepatikana ndani ya siku 90 tangu tarehe ya uchaguzi, lakini CCM kwa maslahi wanayoyajua wao wamekuwa wakiupiga danadana uchaguzi huo.
Mdee alisema hakukuwa na sababu za msingi zilizosababisha uchaguzi huo usifanyike Jumamosi iliyopita.
Mdee alisema kuchelewa kwa uchaguzi huo kumekuwa na madhara makubwa kwa wanancho kwani miradi mingi imesimama.
“Tunamtaka Mkurugenzi atueleze ni lini anatarajia kuitisha uchaguzi... sisi tunataka uchaguzi uitishwe ndani ya siku saba na taratibu zote za matakwa ya kisheria zimeshakiukwa na watu wasioitakia mema nchi hii,” alisema Mdee.
“Kwa sasa tumeambiwa Mkurugenzi hayupo, tumeelezwa ana vikao na sisi tunamsubiri aje alimalize hili suala la umeya wa Jiji.
"Kipindi hiki cha kuelekea bajeti halmashauri zote zinatakiwa kuwa na bajeti na bajeti ya jiji itatengenezwa na nani na kwa maslahi ya nani wakati sisi hatupo?”
Mdee alisema kuna uchafu mkubwa ndai ya Jiji ikiwemo uuzwaji wa Shirika la Uda.
Uchaguzi huo uliokuwa umepangwa kufanyika wiki iliyopita, uligeuka kuwa kama sinema baada ya kuibuka kwa vurugu za kurushiana makonde kati ya wafuasi wa Ukawa na Polisi kufuatia kuahirishwa baada ya zuio la muda Mahakama lilowekwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Zuio hilo la Febriari 5, lililowekwa na Susan Massawe na Saad Khimji dhidi ya Mkurugenzi wa Jiji na Jiji la Dar es Salaam, lilidaiwa kutolewa na Hakimu Mkazi Mkuu Mahakama ya Kisutu, Waliarwande Lema.
Lema amekanusha kutia amri ya kuzia uchaguzi wa Jumamosi iliyopita, uliahirishwa na kufuatiwa na vurugu zilizowakisha Waitara na Mdee katika mahakama hiyo kwa tuhuma za jinai.