Ushindi wa Lulu na Richie kwenye AMVCA 2016 utaziongezea pumzi filamu za Kibongo - MULO ENTERTAINER

Latest

7 Mar 2016

Ushindi wa Lulu na Richie kwenye AMVCA 2016 utaziongezea pumzi filamu za Kibongo

Tuzo za Africa Magic Viewers Choice Awards, ni sawa na Oscars za Afrika. Ndiyo tuzo kubwa zaidi zinazoikutanisha tasnia ya filamu Afrika nzima pamoja.

Utofauti kati ya tuzo za Oscars na AMVCA ni kuwa tuzo za Oscar zinaikutanisha industry ya filamu ya Marekani iliyounganika pamoja, Hollywood bali AMVCA ni tuzo zinazokutanisha industry ndogo ndogo za nchi za Afrika.

Na kwa kiasi kikubwa tuzo za AMVCA ambazo mwaka huu zimetolewa kwa mwaka wa nne zimetawaliwa na Nollywood na kwa mbali tasnia ya filamu ya Afrika Kusini. Kwa kuona hivyo, waandaji walitengeneza tuzo za kikanda na za lugha maalum. Ndiyo maana kuna tuzo ya filamu ya Kiswahili na ya Afrika Mashariki.

Kwa mwaka huu tuzo hizo zote zimekuja Tanzania, ambapo Single Mtambalike maarufu kama Richie ameshinda kipengele cha filamu ya Kiswahili kupitia Kitendawili. Elizabeth ‘Lulu’ Michael alishinda kipengele cha filamu bora ya Afrika Mashariki, kupitia Mapenzi.

Na tumeshuhudia wenyewe kuwa ushindi huu umeshangiliwa zaidi na kurejesha imani katika filamu zetu. Ushindi wa Lulu na Richie unatupa moyo wa kuamini katika kazi za wasanii wetu. Ushindi huu umekuja katika kipindi ambacho tasnia ya filamu ya Tanzania imeshuka kwa kiasi kikubwa katika pande nyingi. Imeshuka kwenye mauzo na usambazaji kiasi ambacho wasambazaji wakubwa wamepunguza kasi ya kusambaza kazi kama zamani na kuwafanya waigizaji wengi kubaki na filamu zao mkononi wasijue namna ya kuzisambaza.

Ni kwasababu ni watanzania wachache wenye muamko wa kutoa fedha mfukoni na kununua filamu za nyumbani. Pengine kwasababu ya utandawazi ambapo tumekuwa ‘exposed’ na filamu bora kutoka Hollywood, imekuwa ngumu sana kuziamini filamu za nyumbani hasa tunapotaka kuzifananisha. Kuna sababu nyingi sana zinazochangia tuziweze kufikia hata asilimia 10 ya ubora wa filamu za wenzetu. Uchumi, teknolojia, ujuzi, elimu, utafutaji na unolewaji wa vipaji kwenye filamu na mambo mengine kibao yanaifanya tasnia yetu iendelee kudoda.

Lakini pengine kama tukiamua kuweka nguvu kwenye vitu vinavyowezekana kama vile kutengeneza filamu zenye story nzuri na zilizobeba uhalisia pamoja na uchaguzi mzuri wa wahusika watakaowasilisha maudhui kwa ufahasa, watanzania wanaweza kushawishika kuzinunua filamu za nyumbani. Inabidi filamu zianze kutengeneza mjadala kama ambavyo muziki wa Bongo Flava umefanikiwa. Kwamba Ray akitoa filamu yake, watu waijadili kwenye mitandao ya kijamii kama ambavyo Diamond au Alikiba na wasanii wengine wakiachia video zao.

Tukirudi kwenye ushindi wa Lulu na Richie kwenye AMVCA, naamini kuwa umepeleka ujumbe Afrika kuwa Tanzania ina kitu. Kama ambavyo kimuziki tunaonekana kuwa vizuri, ni kwa kushinda tuzo kama hizi kunawashtua watu wa pande zingine za Afrika kuwa kumbe nasi tumo.

Cha msingi ni wasanii wetu kuongeza spidi zaidi kwa kutengeneza filamu ambazo hata kama zitatajwa kuwania tuzo hizo, zisiishie tu kuwekwa kwenye vipengele maalum, bali pia kwenye vipengele vya jumla. Tunapenda kuona siku moja Lulu, Kajala, Wema Sepetu, Nisha au Shamsa Ford wanashindana kwenye tuzo moja na Genevieve Nnaji wa Nigeria au Yvonne Nelson wa Ghana.

Tunapenda kuona siku moja Ray, Richie, JB au Hemedy wanashindana kwenye tuzo moja na Ramsey Noah wa Nigeria au Van Vicker wa Ghana.

Mimi ninaamini kuwa ushindi wa Lulu na Richie kwenye AMVCA 2016 utaziongezea pumzi filamu za Kibongo