Uingereza kujitoa Katika Umoja wa Ulaya kwatikisa Ligi Kuu - MULO ENTERTAINER

Latest

27 Jun 2016

Uingereza kujitoa Katika Umoja wa Ulaya kwatikisa Ligi Kuu


London, Uingereza. Klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya England, huenda zikakumbwa na wakati mgumu kutokana na kujitoa nchi hiyo katika Umoja Ulaya, wameonya wataalamu.

“Ada za uhamisho na malipo kwa wachezaji, yanaweza kuongezeka,” alisema Simon Chadwick, Profesa wa Michezo katika Chuo Kikuu cha Salford.

“Klabu zinaweza kusajili wachezaji kwa gharama kubwa na sababu ni kushuka thamani ya Pauni,” Chadwick aliiambia BBC Sport.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka England, Greg Dyke naye alisema uamuzi wa England kujiondoa Umoja wa Ulaya unaweza kusababisha mengi katika Ligi Kuu ya nchi hiyo.

Alisema kuwa matokeo ya kujiondoa EU hakuwezi kuonekana kwa miaka miwili lakini matokeo hasa yataonekana baada ya muda mrefu.

“Itakuwa aibu sana ikiwa wachezaji wakubwa duniani watashindwa kuja hapa, lakini sidhani kama hilo linaweza kutokea. Kama idadi itapungua, itategemea na watakaokuja,” alisema Dyke.

Alisema: “Wasiwasi wangu ni kuwa kutakuwa na kuanguka kwa wachezaji wa Ligi Kuu katika vikosi vya kwanza…tuna anguko na kuteteleka uchumi kwa asilimia 30, hii ni aibu sana.

“Ikiwa wachezaji wa Ligi Kuu wataongezeka, hiyo itakuwa safi. Lakini hatutaki kupoteza kasi ya wachezaji wageni kuja.”

“Uamuzi huo kwa upande mwingine, utasaidia kwa kiasi kikubwa kuwapa nafasi wachezaji chipukizi kupata nafasi katika vikosi vya kwanza katika timu mbalimbali,” alisema Gordon Taylor, Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wachezaji wa Kulipwa.

“Hawa vijana mara nyingi hawapati nafasi, huu sasa ni wakati wao. Wanakuwa na klabu tangu wakiwa na miaka minane hadi 16 na kwa uchache vijana 500 kati ya 600 hawachezi wanapofikia miaka 21,” alisema Taylor.

Uchunguzi wa BBC unasisitiza kuwa matokeo ya England kujiondoa EU kutasababisha mambo mengi katika ligi hiyo ikiwamo ujira wa wachezaji, kuandaa mashindano makubwa na thamani ya jina la Ligi Kuu kupotea.

Nick Chadwick, mchezaji wa zamani wa Manchester United alisema: “Soka yetu iliyokuwa ikitamba kwa muda mrefu, itaathiriwa na Umoja wa Ulaya.

“Sasa ni kutengeneza njia mpya na mawazo mapya kuelekea kule ambako hatujafahamu jambo la kufanya na hiyo inaweza kuwa kwa miaka mitano hata 10.”

Alisema: “Kitu cha kwanza tutakachokiona hapa ni hili la usajili. Tulichokiona kwa saa chache ni kuporomoka kwa kiasi fulani usajili.

“Wachezaji watashindwa kuja England ikiwa thamani ya mishahara yao itaanguka,” aliongeza Chadwick.


Hata hivyo, alisema kuwa Ligi Kuu itaendelea kuwa ligi kubwa na bora yenye mafanikio na ushindani nyumbani na duniani bila kujali matokeo ya kura ya uamuzi.

“Hakika, tutaendelea kushirikiana na serikali na vyombo vingine na wadau.”

Baadhi ya wadau walisema kuwa kujindoa kwa England kutapunguza uhuru wa wachezaji kuhamia sehemu moja na nyingine.

Uchambuzi wa BBC mapema Machi wakati wa vuguvugu hilo unaonyesha kuwa katika England na Ligi Kuu ya Scotland, wachezaji 332 watakosa sifa za kuchezea timu hizo.

Klabu ya Scotland ya Hamilton Academical italazimika kubadili sera ya kusajili, na kocha Martin Canning alisema kuwa wachezaji wanane wataathirika huku urahisi wa kuja England ukiwa kwa wachezaji nje ya Umoja wa Ulaya.

“BBC ilisema kuwa mchezaji kama N’Golo Kante wa Leicester, ni wazi atashindwa kuchezea timu hiyo hadi afuate utaratibu za kibali,” alisema Chadwick