Kwanza nikiri kuwa, Diamond ana fursa nyingi za wazi wazi ambazo ameziacha tu zipite. Kwa umaarufu aliojikusanyia hadi sasa katika bara zima, alipaswa kuwa na miradi mingi chini ya jina lake ambayo ingekuwa inamuingizia mamilioni ya fedha, ukiacha zile anazopata kutokana na muziki wake.
Lakini bado hajachelewa na kwakuwa ukubwa wake unaanza kuizidi nguvu timu yake, mambo mengine yatakuja pole pole, na uzuri tayari tumeanza kuyaona. Nafahamu kuwa aliwahi kuonesha interest ya kuanzisha clothing line yake ya WCB ambayo hata hivyo aliishia kutoa bidhaa chache tu zilizovaliwa na watu wa karibu na hazikuwahi kuingia sokoni kwa ukubwa uliotarajiwa. Hicho ni kitu ambacho huenda akawa amekiweka pending kwa muda.
Leo nichukue fursa kumpongeza kwa kuonjesha mradi wake mkubwa wa perfume aliyoipa jina la utani, Chibu. Ni hatua kubwa sana, tena kutoka kwa msanii wa Tanzania. Sina idadi kamili ya celebrity wa Afrika wenye bidhaa ya aina hiyo, na kama wapo basi ni wachache sana. Tumezoea perfume kuwa ni kitu kinachofanywa na mastaa wakubwa duniani kama Nicki Minaj, Beyonce, Diddy, David Beckham na wengine, hivyo kwa msanii wa Tanzania kuja na kitu kama hicho na tena kinachoonekana kuwa si cha mzaha, si suala la kuchukulia poa.
Diamond anastahili pongezi kwa uthubutu huo na kuionesha Afrika kuwa, Mtanzania anaweza kufanya kitu kikubwa. Ujio wa perfume yake, ni udhihirisho tosha kuwa sasa muimbaji huyo anazidi kujitambua kuwa brand yake imekuwa kubwa na anaingia rasmi kwenye biashara ya muziki yenye matawi mengi. Katika daraja analoingia sasa, Diamond ataanza kuifaidi fedha wanayoifaidi mastaa wakubwa katika nchi zilizoendelea.
Ametambua kuwa kwa hatua aliyofikia, si muziki wake pekee unaouza, bali ni jina lake ndilo lenye thamani zaidi ya kitu chochote kwa sasa. Ametambua kuwa, amefika katika anga ambazo hamlazimu tena kutegemea muziki, endorsement na show peke yake, bali kwa mtaji wa jina lake na wafuasi wake, anaweza kutengeneza fedha kubwa zaidi.
Hatua hiyo inazidi kumweka katika ligi ya juu inayochezwa na wanamuziki wenzake nguli Afrika. Na kwakuwa si nguli wengi wa level yake wana mradi kama huo, inampa upekee zaidi na kuipa heshima Tanzania. Na pengine jambo kubwa zaidi, ni ari ya uthubutu anayoipandikiza kwa mastaa wengine wa Bongo na kuwatengenezea njia za kupita watakapo kufanya uwezekazaji wenye sura ya ukubwa kama huo anaoenda kuufanya punde.
Heko kwa Diamond na bila shaka perfume yake itapata mapokezi mazuri nje na ndani ya Afrika.
21 Nov 2016
New