Jina hilo limetokana na eneo ambalo madini hayo yalipatikana, Merelani (Mererani) katika milima ya Lelatema katika wilaya ya Simanjiro katika eneo la Manyara. Madini hayo yaligunduliwa na wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Kiteknolojia cha Michigan cha Marekani, makavazi ya historia asilia ya London, chuo kikuu cha Di Firenze cha Italia na makavazi ya historia asilia ya Smithsonian ya Washington.
Wataalamu sita waliofanya uchunguzi, kwenye makala iliyochapishwa kwenye jarida la Minerals (Madini) wanasema madini hayo yana vipande vinavyofanana na sharubu vya rangi ya kijivu vya urefu wa milimita moja hivi, ingawa kuna baadhi vyenye urefu wa hadi mililita 12.
Madini hayo yanakaribiana na madini ya zoisite (aina ya tanzanite), prehnite, stilbite, chabazite, tremolite, diopside, quartz, calcite, graphite, alabandite na wurtzite.
Madini hayo yalitambuliwa mara ya kwanza mwaka 2012 na Simon Harrison na Michael Wise, bila wataalamu hao kuyafahamu vyema, pale walipogundua vitu vilivyoonekana kama nyaya ndogo zilizokuwa zimedunga na kuingia ndani ya vipande vya madini ya chabazite.
Baadaye uchunguzi zaidi ulifanywa na ikagunduliwa kwamba yalikuwa madini tofauti.