Viongozi na Wafuasi 10 wa Chadema Jijini Mbeya Wakamatwa na Polisi - MULO ENTERTAINER

Latest

13 Sept 2018

Viongozi na Wafuasi 10 wa Chadema Jijini Mbeya Wakamatwa na Polisi

Viongozi na Wafuasi 10 wa Chadema Jijini Mbeya Wakamatwa na Polisi
Viongozi na wafuasi 10 wa Chadema jijini Mbeya wamekamatwa na polisi usiku wa kuamkia leo wakiwa wamelala kwenye ngome yao waliyoweka kwa ajili ya kushiriki kampeni za uchaguzi mdogo kata ya Iwambi.

Mwenyekiti wa Chadema Mbeya Mjini, Obadi Mwaipalu ameiambia Mwananchi Digital leo kwamba,  usiku wa saa 10:00 polisi wakiwa na silaha za moto walivamia ngome yao wakiwa wamelala na kuwakamata.

 “Jana (juzi) walikwenda usiku wa saa 10:00 wakamkamata mkuu wa kambi yetu Mwansile, tena leo usiku wa saa 10:00 polisi wakiwa na silaha wamekwenda na kuwakamata watu wetu wakiwa wamelala. Mbaya zaidi wamewafanyia ukiukwaji wa haki za binadamu, wamewakamata kinamama na kuwatoa nje wakiwa uchi kabisa pia wapo kinamama wenye watoto wadogo lakini wamewakalisha nje kwenye baridi.”

 “Hadi sasa hatujui sababu za kuwakamata watu wetu na hatupewi maelezo ya kujitosheleza, lakini tunajua hizi zote ni njama za wapinzani wetu (CCM) baada ya kuona wameshikwa kila kona hawana pa kutokea na sasa wameamua kutumia polisi kutupunguza nguvu, lakini tunasema hilo halitusumbui tutapambana hadi dakika ya mwisho,” alisema.

 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ulirich Matei alipopigiwa simu ili kutolea ufafanuzi  suala hilo hakupokea, badala yake alituma ujumbe mfupi akisema yupo kwenye kikao na atamtafuta mwandishi baadaye.