Ruge wa Clouds FM Amsifia Ruby, Adai Ana Kipaji cha Hali ya Juu - MULO ENTERTAINER

Latest

21 Nov 2016

Ruge wa Clouds FM Amsifia Ruby, Adai Ana Kipaji cha Hali ya Juu

Mwanzilishi wa THT na Mkurugenzi wa vipindi na uzalishaji wa Clouds FM, Ruge Mutahaba, amesema licha ya Ruby kuwa na tofauti naye na kujiondoa kutoka kwenye usimamizi wake, hawezi kushuka kimuziki sababu ana kipaji cha hali ya juu.

Miezi miwili iliyopita, Ruby alijiondoa kwenye usimamizi wa THT na kukataa kutumbuiza kwenye tamasha la Fiesta hali iliyotafsiriwa kuwa hilo linaweza kuwa anguko lake. Hata hivyo bado muimbaji huyo anaendelea kuwika ikiwa ni pamoja na kushiriki kwenye kipindi cha Coke Studio Africa ambako amejinyakulia sifa za kutosha.

Akiongea na mtangazaji wa Mashujaa FM ya Lindi, Baby Dinny, Ruge amesema kipaji cha Ruby ni ‘unstoppable’ na kwamba kama akipata waandishi wengine wazuri atafika matawi ya mbali.

“Mimi naamini Ruby ana kipaji sana. Binafsi ana kipaji cha ukweli kabisa wala sio uongo,” alisema Ruge. “Kama atashuka labda itakuwa ni mambo yake tu mwenyewe lakini sidhani kama kuna namna kipaji chake kitashuka,” aliongeza na kumshauri kuwa apate watunzi wengine wazuri wa kumsaidia. Anadai kuwa nyimbo zake tatu, Na Yule, Forever na Sijutii, ziliandikwa na yeye akishirikiana na Amini na Barnaba.

Kwa upande mwingine, Ruge amesema haoni kama kuna tatizo Ruby kuondoka THT kwakuwa tofauti na wengine wanavyodhani, THT si label bali ni kama chuo ambacho wasanii mbalimbali hunolewa.

“Yeye ameona yuko tayari kivyake kwenda kwenye sehemu anayoweza kupata maslahi zaidi, ndio hivyo tu, kwahiyo sioni kama kuna shinda,” amesisitiza Ruge.

Pia amedai kuwa muda wowote ambao muimbaji huyo atahitaji ushauri kutoka kwake, milango iko wazi kwakuwa bado ataendelea kumchukulia kama mdogo wake. Msikilize Hapa: