LICHA ya takwimu za hivi karibuni kuonesha uchumi wa Taifa pamoja na Pato la Taifa vimekuwa vikikua kwa kasi na kuifanya Tanzania kuwa moja ya nchi zenye uchumi imara, kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imedai kuwa uchumi wa Tanzania umeyumba.
Kambi hiyo imetaja baadhi ya maeneo yanayothibitisha hilo kuwa ni mikopo inayotolewa na benki za biashara kwenye sekta binafsi kuwa imeshuka katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Fedha na Uchumi, Halima Mdee alisema mikopo hiyo imefikia Sh bilioni 1,167.2 ikilinganishwa na ongezeko la Sh bilioni 1,577.5 la mwaka 2015 katika kipindi kama hicho.
“Hii maana yake sekta binafsi imekosa Sh bilioni 410.3 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2016. Hali hii imefanya mzunguko wa sarafu na noti mikononi mwa watu kushuka kutoka asilimia 188.8 Desemba 2015 na kufikia asilimia 6.7 Julai mwaka 2016,” alieleza.
Alisema kwa mujibu wa taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT), amana za wateja katika benki zilipungua kutoka Sh trilioni 20.52 Desemba 2015 hadi kufikia Sh trilioni 20.24 Juni mwaka 2016.
Akichangia mapendekezo ya mpango huo wa maendeleo, Mbunge wa Sikonge, Joseph Kakunda (CCM) alisema takwimu zinaonesha asilimia 53 ya viwanda vikubwa nchini vipo kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Kagera na Arusha, uwiano ambao si mzuri na kutaka viwanda viwepo kwenye mikoa mingine pia.
Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa hivi karibuni na Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS), Dk Albina Chuwa, katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka huu, Pato la Taifa limeendelea kukua kwa kasi ya asilimia 7.9 ikilinganishwa na asilimia 5.8 ya robo ya pili ya mwaka jana.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Benno Ndulu alisema ukuaji wa Pato la Taifa katika nusu ya kwanza ya mwaka ya Januari hadi Juni, umeongezeka na kufikia asilimia 6.7 kutoka asilimia 5.7 kwa nusu ya kwanza ya mwaka 2015.