Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Makao Makuu ya Nchi, Dodoma.
Akizindua safari hizo leo amesema safari hizo zitawezesha wafanyabiashara na wananchi wengine kutoka Dodoma na kwenda katika maeneo mengine kwa urahisi.
“Tuna ndege nzuri. Tuzitumie kwenda katika maeneo mengine kwani gharama zake ni nafuu. Kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam ni sh. 165,000, kwenda na kurudi ni sh. 299,000,” amesema.
Amesema ndege nyingine kama hiyo inatarajia kuwasili nchini Juni mwaka huu jambo ambalo litaongeza idadi ya safari za ndege hizo nchini na maeneo mengine ya nchi jirani.
Kwa upande wake Kaimu Mtendaji Mkuu wa ATCL. Kapten Richard Shaidi ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali kwa ujio wa ndege hizo na kwamba hiyo ni moja ya mikakati ya Mheshimiwa Rais Dkt. Magufuli ya kufufua ATCL.
“Hivi karibuni tunaanza kwenda nchi jirani. Mwakani tutapata ndege nyingine kubwa itakajayokuwa inafanya safari za masafa ya kati na ya mbali” amesema.
Aidha, Mwenyekiti wa Bodi ya ATCL, Bw. Emmanuel Korosso amesema hivi karibuni shirika hilo linatarajia kuanza safari za kwenda katika miji ya Tabora, Songea, Mtwara, Mpanda, Mafia na Jiji la Tanga.
Akizungumzia kuhusu safari za Dodoma amesema zitafanyika mara mbili kwa wiki, siku ya Ijumaa na Jumatatu. Hata hivyo wanatarajia kuongeza safari hapo baadae.
Naye Spika wa Bunge, Mheshimiwa Job Ndugai ametoa wito kwa wakazi wa Dodoma kutumia vizuri fursa hiyo ya safari za ndege za ATCL kwa kuwa utawawezesha kusafiri kwa muda mfupi tofauti na vyombo vingine vya usafiri.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Bw. Jordan Rugimbana ameshukuru kwa uanzishwaji wa safari hizo kwa kuwa zitarahisisha kutoka katika Makao Makuu ya nchi na kwenda katika mikoa mingine nchini.