TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki anashikiliwa na Jeshi la Polisi
kwa madai ya kutoa maneno ya uchochezi kuhusu kuwepo kwa njaa nchini.
Hatua hiyo inafuatiwa na Serikali ya Rais John Pombe Magufuli kupinga
kuwepo kwa njaa nchini na kwamba, wafanyabiashara wachache wamekuwa
wakishirikiana na baadhi ya watu kueneza taarifa hizo.
Simon Siro, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam leo amewaambia
waandishi wa habari kwamba, wanamshikilia Lissu kutokana na tuhuma hizo.
Si mara ya kwanza Lissu ambaye ni Mwanasheria wa Chama cha Demokrasia na
Maendeleo (Chadema) kukamatwa kwa madai yanayofanana na hayo.
Miongoni mwayo ni tarehe 22 Desemba mwaka jana ambapo Lissu aliachwa
baada ya saa kadhaa kukamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi katika
Kituo Kikuu cha Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa madai ya kutumia jina
la Rais Magufuli kwa dhihaka kwa kumwita rais mtukufu.
Alianza kuulizwa kuhusu mkutano wake na waandishi wa habari
alipozungumzia kupotea kwa Ben Saanane, aliyekuwa msaidizi wa karibu wa
Mbowe “aliitwa kuhojiwa juu ya Press conference aliyofanya na
kuzungumzia suala la Saanane lakini pia wamemuhoji anamaanisha nini
kumwita Rais John Magufuli jina la “Mtukufu.”
Lissu amekuwa akimtaja Rais Magufuli kama “mtukufu” mara kadhaa tangu
aliposhitakiwa kwa kutamka kuwa “Dikteta uchwara anapaswa kupingwa kwa
nguvu zote.”
Lissu alikamatwa jana jioni mjini Dodoma katika vianja vya bunge na kusafirisha moja kwa moja hadi jijini Dar es Salaam.
Baada ya kukamatwa kwake, Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema-Taifa alieleza kutojua sababu za kukamatwa kwake.
Jeshi la Polisi limeeleza kuwa, Lissu anaendelea kuhojiwa kutokana na tuhuma hizo.