NAIBU Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, `amemuumbua Naibu Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Dk. Hamis Kigwangalla
baada ya kukanusha taarifa ya bohari za dawa kuwa haziko chini ya
kiwango.
Naibu Spika huyo alilazimika kutoa maelekezo kwa serikali kuangalia
Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG)juu ya
ubovu wa bohari za dawa nchini na kuzifanyia kazi kasoro kama
watazikuta.
Hatua hiyo ya Dk. Tulia ilitokana na Dk. Kigwangalla kukanusha taarifa
ya bohari za dawa kuwa chini ya kiwango zilizotolewa na Mbunge wa Viti
Maalum (CUF), Halima Ally Mohamed.
Mbunge huyo akiuliza swali la nyongeza, alisema kwa mujibu wa taarifa ya
CAG ya mwaka 2014/15, kuna bohari zisizo na viwango na kutaka kujua
msimamo wa serikali ili kuhakikisha afya za Watanzania.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla alisema: “Kwanza, naomba nikanushe
vikali sana kwamba kuna bohari za dawa zisizo na viwango. Hiyo ni ripoti
ya CAG na hii ni taarifa ya serikali. Kwa hiyo naongea kama serikali
kwa mamlaka kamili niliyopewa.”
Alisema bohari zilizopo ni za viwango vya hali ya juu na vimethibitishwa
na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO), na zinakaguliwa kila baada ya
miaka mitano na dawa haziwezi kutunzwa kwenye bohari zisizo na viwango
kwa sababu zitaharibika.
“Dawa ni ‘high value items’ na hatuwezi kuzitunza ovyo, hivyo kwa sababu
tunazitunza kwa gharama kubwa na ndiyo maana katika utunzaji,
usambazaji mpaka katika kituo cha afya kijijini, kuna mnyororo
uliokamilika unaozingatia viwango vya ubora,” alisema Dk. Kigwangalla.
Kufuatia majibu hayo, Dk. Tulia alisema: “Mheshimiwa Naibu Waziri, kwa
kuwa mbunge ameuliza taarifa zinazotokana na Ripoti ya CAG, serikali
iangalie katika hiyo ripoti inasema nini ili kama alichosema mbunge kipo
sawasawa ama hakipo sawasawa.”
Alisema kama kinachosemwa kipo kwenye ripoti, Wizara ya Afya iliangalie suala hilo.
Baada ya agizo hilo, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee,
Watoto, Ummy Mwalimu, alisimama na kusema wamelipokea swali hilo na
watalifanyia kazi.
Katika swali la msingi, Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje,
aliishauri serikali kuiwezesha Bohari ya Dawa nchini (MSD) kuwa na fungu
maalum kutoka Hazina.
Akijibu swali hilo, Dk. Kigwangalla alisema MSD haiwezi kupewa fungu la moja kwa moja bila kupitia Wizara ya Afya.