Mpya Zakunyapia Nyapia..Kisa Wema Kulala Lupango, Mama Wema Hali Mbaya
Hali ni tete! Baada ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda
kutaja majina ya wanaotuhumiwa kujihusisha biashara na matumizi ya
madawa ya kulevya wakiwemo mastaa ambapo Ijumaa iliyopita baadhi yao
walitii wito na kufika katika Kituo Kikuu cha Polisi, Dar ‘Sentro’ kwa
ajili ya mahojiano akiwemo Wema Isaac Sepetu, mama yake mzazi, Mariam
Sepetu anaelezwa kuwa katika hali mbaya kutokana na mwanaye huyo kulala
lupango.
Chanzo makini kilicho karibu na mama Wema kilieleza kuwa, baada ya
Ijumaa, Wema kwenda kuhojiwa Sentro na kulala lupango, hali ya hewa
ilibadilika nyumbani kwa mama yake, Sinza-Mori, Dar kwani mzazi huyo
presha ilikuwa juu na kusababisha akeshe akilia usiku kucha.
“Yaani siku ya Ijumaa ambayo Wema na wenzake waliotajwa walikwenda
kuhojiwa Sentro kisha kulala lupango, ilikuwa ni siku ngumu sana kwa
mama Wema kwani alikuwa akilia siku nzima na usiku wake hakulala kabisa
hadi kunakucha.
“Alfajiri ya Jumamosi, ilibidi ndugu zake wamfuate na kumchukua,
haikujulikana kama walimpeleka hospitali au wapi lakini hali yake
ilikuwa mbaya huku akimlilia mwanaye Wema ambaye alilala lupango ,”
kilisema chanzo hicho.
WIKIENDA KWA MAMA WEMA
Baada ya habari hizo kutua kwenye meza ya Wikienda, wanahabari wetu
walitinga nyumbani kwa mama Wema na kukutana na kijana ambaye alifungua
geti kwa nafasi ndogo huku akiwa anaonesha wasiwasi mkubwa na
kutetemeka.
Kijana huyo alipoulizwa kama mama Wema alikuwepo alijibu hakuwepo.
Alipoulizwa alikokwenda alisema: “Alichukuliwa alfajiri na ndugu zake.”
Alipoulizwa hao ndugu zake walimpeleka wapi alijibu: “Sijui’.
Alipoulizwa hali yake kiafya ilikuwaje, alifunguka: “Mama yuko kawaida
tu.”
Alipoulizwa juu ya Wema kutoka lupango au la, alijibu:
“Kuhusu Wema haishi hapa, yeye anaishi Ununio.”