Tundu Lissu Abaini Mbinu Chafu kwa Chama Fulani Kuweka Mgombea Urais TLS..!!! - MULO ENTERTAINER

Latest

12 Feb 2017

Tundu Lissu Abaini Mbinu Chafu kwa Chama Fulani Kuweka Mgombea Urais TLS..!!!



Mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki kupitia chama hicho, Tundu Lissu amezungumzia hatua yake ya kujitosa kuwania urais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS).

Mosi, Lissu amesema amepata msukumo kutokana na kauli ya rais John Magufuli kuwa kuna kampeni zimeanza za kumuondoa rais wa sasa wa TLS na zinaendeshwa na chama fulani ambacho kimeweka mgombea wake.

Pili, akasema Lissu ni kauli kuwa mawakili wanaotetea wauza dawa za kulevya nao wakamatwe wawekwe ndani.

“Sikuwa na mpango wa kugombea lakini the moment (wakati) aliposema, nikasema sasa nitagombea urais wa TLS,” amesema mbunge huyo.

Rais alitoa matamko hayo katika sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria iliyofanyika mapema mwezi huu kwenye uwanja wa Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam.

Lissu amesema TLS imepoteza mwelekeo na nafasi yake katika jamii kwenye masuala ya kisheria, hasa kushindwa kukemea vitendo vya uvunjifu na ukiukaji wa Katiba na sheria unaofanywa na viongozi.

“Chama cha wanasheria kinatakiwa kiwe cha kwanza kupiga kelele sheria za hovyo zinapotungwa, kinatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea vitendo vya ukiukaji wa Katiba na sheria vinavyofanywa na watu wenye mamlaka lakini Law society ya kwetu imekaa kimya,” amesema.

Kuhusu msimamo wake wa kisiasa na chama hicho endapo atapata nafasi hiyo, Lissu amesema masuala ya kisheria hayana uhusiano na vyama vya kisiasa na kwamba chama hicho kipo kwa ajili ya kulinda na kusimamia utawala wa sheria.

Pia, amesema kama chama chake kitakuwa na msimamo sawa na misingi ya chama hicho katika kutetea utawala wa kisheria, si tatizo na kwamba, ikiwa kitakuwa na msimamo tofauti katika mambo ya msingi, hakina budi kukosolewa.

“Sigombei ili kuipeleka Chadema ndani ya TLS. Masuala haya yanatuhusu sisi wote kujua mambo yanapoharibika, kuona sheria zinapokiukwa na kuona sheria mbovu zinapotungwa,” alisema.

Ofisa Maboresho ya Sheria wa TLS, Mackphason Buberwa amesema mchakato wa kupata wagombea umeshakamilika na waliopitishwa na kamati ni watano.

“Taratibu zimekamilika, kilichobaki ni wagombea kuandaa kampeni zao kabla ya Machi 18 siku ambayo uchaguzi utafanyika mjini Arusha,” amesema Buberwa.

Wagombea wengine ni Francis Stola, Lawrance Masha, Victoria Mandali na Godwin Mwapongo. Uchaguzi huo umepangwa kufanyika Machi 18 jijini Arusha ambako zaidi ya mawakili 6,000 wanatarajiwa kuhudhuria.