Katibu mkuu wa wizara ya maji Prof: Kitila Mkumbo amelitaka shirika la
maji safi na taka nchini DAWASCO kuhakikisha wanawekeza sana kwenye
usambazaji wa maji kwani ni aibu kwa jiji la Dar es salaam kuwa na
maeneo ambayo hayana maji.
Prof: Kitila Mkumbo ametoa maagizo hayo jana jijini Dar es salaam wakati
alipofanya ziara katika shirika hilo na kukutana na watendaji wakuu wa
DAWASCO pamoja na watendaji wakuu kutoka Mamlaka ya maji safi na taka
jijini Dar es salaam DAWASA.
“Pamoja na kazi nzuri mnayofanya ya kuhakikisha upatikanaji wa maji
hakikisheni mnaongeza kasi ya usambazaji wa huduma hii muhimu kwa
wananchi kwa kufanya hivyo mtakuwa mnatendea haki dhana ya kuwa
mnaongoza kwa mapato lakini pia mnatoa huduma stahiki kwa wananchi”.
Alisema Prof. Kitila
Pamoja na hayo amewasii wateja wote wa DAWASCO kutii agizo la Mhe. Rais
kwa kulipia huduma wanazozipatiwa ili kuziwesha mamlaka hizo kutekeleza
majukumu yake kwa ufanisi.
Prof: Mkumbo pia amelitaka shirika hilo kukamilisha miradi ya maji
katika maeneo ambayo mpaka sasa inaonekana haijakamilika kwa lengo la
wananchi kupata maji.