MCHUNGAJI David Mabushi wa Kanisa la IEACT lililopo katika Manispaa ya
Shinyanga, amesema kanisa linamuunga mkono Rais John Magufuli kwa yale
anayoyatekeleza kulinda rasilimali za umma, huku akimfananisha kiongozi
mkuu huyo wa nchi na Nabii Musa, aliyekuja kuwakomboa wana wa Israel.
Mchungaji Mabushi alisema hayo juzi ofisini kwake wakati akizungumza na
gazeti hili baada ya kumalizika kwa ibada ya Sikukuu ya Pasaka, huku
akieleza kuwa Rais Magufuli amedhamiria kuyafanya aliyokuwa akiahidi
katika kipindi cha kampeni wakati wa Uchanguzi Mkuu mwaka 2015 hata
Watanzania wakamwamini na kumchagua kuliongoza taifa.
Mabushi alisema kanisa lake linamuunga mkono Rais Magufuli kwa juhudi na
kazi zote, anazozifanya kulinda rasilimali za nchi hii zisizidi
kuwanufaisha Watanzania wachache. Kiongozi huyo wa dini, alisema
utekelezaji wa ahadi alizotoa Rais Magufuli wakati akigombea wadhifa huo
pamoja na hatua anazochukua kiutendaji ni mambo yanayoleta tija na
ukombozi kwa Watanzania, kama Nabii Musa alivyokuja kuwakomboa wana wa
Israel.
Alisema miongoni mwa masuala yaliyokuwa yakilalamikiwa na Watanzania
wengi ni pamoja na kuwepo kwa mikataba mibovu ya migodi na mchanga,
kusombwa kupelekwa nje ya nchi ukiwa na rasilimali nyingi. Hivyo,
alisema kitendo cha kuzuia usafirishaji wa mchanga huo na kuunda tume
mbili za kuchunguza ili kujiridhisha kuhusu vilivyomo katika mchanga huo
ni cha kijasiri, kwani kimelenga kujiridhisha na hali halisi, na
kuondoa manung’uniko kwa kuwa ukweli utakuwa wazi.
“Lakini ninashangazwa na baadhi ya Watanzania wamekuwa kama
anachokifanya Rais kukemea uovu, ubadhirifu ufisadi na rushwa sio
walichokuwa wakikisema kipindi cha nyuma…Wengi hawataki kupaza sauti
kumuunga mkono na sasa sisi tunamuombea kwa Mungu huku tukimshauri
amuachie Mungu kila jambo kwa kuwa ameamua kuwatumikia wananchi
wanaonyonywa rasilimali zao,” alisema Mchungaji Mabushi.