Hatimaye kundi la vichekesho lililojipatia umaarufu mkubwa nchini la
Orijino Komedi, limefikia mwisho kwa kusambaratika, huku chanzo
kikidaiwa kuwa ni mmoja wa memba wake mwenye mbwembwe nyingi, Silvery
Mujuni, maarufu kama Mpoki a.k.a Mwarabu wa Dubai, Risasi Mchanganyiko
limenyetishiwa.
Kwa mujibu wa chanzo kilicho karibu na kundi hilo ambalo halijarusha
kazi zake hewani kwa muda mrefu sasa, limeingia katika hatua hiyo, baada
ya mmoja wa memba wake, kukiuka makubaliano, kitu kilichosababisha wote
waamue kufanya mambo kivyao.
Inadaiwa kuwa hapo awali, kulikuwa na maazimio ya kila mmoja kuleta
kundini, makubaliano yoyote ya kazi kibiashara ili mapato
yatakayopatikana, wagawane wote.
“Walijua kuwa kazi zao kama kundi ziliwavutia kampuni na mashirika,
lakini wakafahamu pia kuwa wakati mwingine siyo rahisi kundi kuingia
mikataba, kwamba wapo ambao wangeweza kuvutiwa na mmoja wao, hivyo
ikitokea namna hiyo, basi aliyepata dili hilo, alilete kundini, ambako
yeye atapewa asilimia kubwa, huku wenzake nao wakipata kidogokidogo,”
kilisema chanzo hicho.
Chanzo hicho kikaongeza kuwa, utaratibu ukawa ni huo na kila kitu
kikaonekana kwenda vizuri, hadi Mpoki alipokuja ‘kutibua’ baada ya
kupata dili kutoka kampuni moja ya simu, lakini kwa mshangao wa wenzake,
hakupeleka kundini makubaliano yake.
“Watu walishtukia tu tangazo linaruka hewani, alipoulizwa imekuaje,
akawa haeleweki, ndipo wenzake nao wakaamua kila mmoja kufanya kivyake
na hapo ndipo kutokuelewana kukatokea,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya kupata ubuyu huo, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Mpoki, ambaye
kwa sasa ni mtangazaji katika Kituo cha Redio cha EFM, ambapo baada ya
kuelezwa kuhusu tuhuma hizo, alihoji;
“Hayo maneno kakuambia nani? Pale kwenye kundi letu tupo wengi au wao
ndiyo wamekuambia? Mimi siwezi kujibu hiyo kitu na huwezi kunilazimisha
kujibu.”
Risasi Mchanganyiko pia lilijaribu kuwafikia wanakikundi wengine ili
kupata ukweli wa habari hizo na safari hii, walimtafuta Lucas Lazaro
Mhuvile, anayefahamikazai di kama Joti, ambaye baada ya kuulizwa kuhusu
kilichotokea kwenye kundi lao, mahojiano na mwandishi yalikuwa kama
ifuatavyo;
Joti: Lazima uniambie kwanza ni nani aliyekuambia habari hizo.
Mwandishi: Lakini maadili ya kazi yetu hayaruhusu mimi kutaja chanzo
changu, nadhani wewe ungejibu tu vile unavyojua juu ya jambo hilo.
Joti: Mimi siyo mwandishi, ninachotaka utuite mimi na yeye aliyekuambia
hizi habari, tukae tuambizane vinginevyo siwezi kukujibu kwamba ni kweli
au siyo kweli.
Gazeti hili lilimfikia pia mchekeshaji mwingine maarufu wa kundi hilo,
Isaya Mwakilasa ‘Wakuvanga’ ambaye baada ya kuelezwa kusudio la kupigiwa
simu, alisema hivi; “Unataka nikupe habari hovyohovyo au unataka nikupe
kitu kizuri uandike? (Mwandishi alipomweleza kuwa anahitaji kitu
kizuri, akamwambia), basi nitafute wakati mwingine kwa sababu hivi sasa
nipo katika kazi muhimu.”
Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ hakupokea simu yake licha ya
kupigiwa mara kadhaa na hata ujumbe mfupi wa simu hakujibu, kama
ilivyokuwa kwa Mark Regan.
Hata hivyo, kiongozi wa kundi hilo, Sekioni David, maarufu kama Seki, alizungumza na Risasi Mchanganyiko .
“Kundi bado lipo ila kwa sasa liko mapumzikoni. Unajua, shoo ya mwisho
tulifanya Septemba 2015, baada ya pale tukaingia katika kampeni, ila
kazi ni ngumu na pia tokea tumeanza, hatukuwahi kupumzika, watu
wanatakiwa wapumzike ili wapate ubunifu mpya.
“Kifupi ni kuwa tupo likizo tangu ile 2015, nadhani tutaendelea mwishoni
mwa mwaka huu, kwa hiyo mwakani kundi linarejea barabarani kama
kawaida, hiyo habari kuwa tumesambaratika siyo kweli, hivi sasa watu
wako mashambani wanashughulika na kilimo.”