NI katika mkutano wa waandishi wa habari katika Umoja wa Mataifa
ulioandaliwa na Korea Kaskazini, ndipo unapoweza kumsikia
mwanadiplomasia akiwatakia wanahabari sikukuu njema ya mwisho wa wiki
halafu kutoa onyo la vita ya kinyuklia.
Katika miongo ya karibuni Korea Kaskazini imekuwa ikitoa vitisho vya
mara kwa mara juu ya kuzuka kwa vita baina yake na Marekani, lakini
utawala wa Rais Donald Trump ulitangaza kumalizika kwa zama za sera ya
uvumilivu dhidi ya Pyongyang. Balozi mdogo wa Korea Kaskazini katika
Umoja wa Mataifa, Kim In Ryong aliitisha mkutano wa haraka wa waandishi
wa habari jijini New York.
Mkutano huo uliandaliwa masaa kadhaa baada ya Makamu wa Rais wa Marekani
Mike Pence kutembelea eneo lisiloruhusiwa shughuli za kijeshi katika
mpaka wa Korea Kaskazini na Kusini. Pence alionya kwamba Korea Kaskazini
isitake kuijaribu nchi yake “au nguvu za majeshi yetu.”
Huko New York, Korea Kaskazini ilirusha moto wa maneno. Balozi huyo
alilaani kuongezeka kwa uwepo wa majeshi ya Marekani katika bahari
karibu na peninsula ya Korea, pamoja na shambulizi la kombora
lililofanywa dhidi ya Syria.
Kim alisema, “Hii imeleta hali ya hatari ambayo inaweza kusababisha vita
ya kinyuklia kuibuka muda wowote katika peninsula na inatishia kupotea
kwa amani na usalama wa dunia.”
Wakati waandishi katika Umoja wa Mataifa wamewahi kusikia lugha kama
hiyo kutoka kwa Korea Kaskazini, maneno yaliyotolewa juziJumatatu
yalikuwa ni makali zaidi.
Akisoma taarifa iliyoandaliwa kwa ajili ya waandishi wa habari, alisema,
“Marekani inataka kuharibu amani na ustawi wa dunia kwa kufanya mambo
ya kihuni kama kufanya uvamizi wa taifa huru ni jambo jema ambalo lina
lengo la kulinda ustawi wa ulimwengu na inajaribu kufanya hivyo katika
peninsula ya Korea pia.”
Kim alisema kuwa nchi yake ipo tayari kuchukua hatua dhidi ya hali
yoyote ya kivita kutoka kwa Marekani. Shambulizi lolote la makombora au
nyuklia litakalofanywa na Marekani litajibiwa kwa nguvu ile ile,”
alisema.
Ni wazi kwamba Umoja wa Mataifa una wasiwasi. Msemaji wake Stephane
Durarric aliwaambia waandishi wa habari, “Tunasikitishwa na kuongezeka
kwa hali ya wasiwasi ambayo tunaishuhudia katika peninsula ya Korea.
Tunazitaka pande zote kutumia njia za kidiplomasia kumaliza tatizo
hili.”
Korea Kaskazini ilifanya jaribio la kombora ambalo lilishindwa mwisho wa
wiki hii. Dujarric alisema, “Nadhani jaribio la karibuni kabisa ambalo
limefanyika mwisho wa wiki hii linatia wasiwasi. Tunaitaka Korea
Kaskazini kuchukua hatua zote muhimu ili kutuliza hali ya mambo na
kurudi kwenye meza ya mazungumzo ya kuachana na mpango wake wa kutafuta
silaha za kinyuklia.”
Korea Kaskazini imekasirishwa kwamba Baraza la Usalama la Umoja wa
Mataifa litaitisha kikao baadae mwezi huu kuzungumzia suala hilo, kikao
ambacho kitaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Rex Tillerson.