MUZIKI ni sanaa pana inayohitaji zaidi akili iliyotulia ili kuifanya
kuwa bora na isiyokufa. Ni wanamuziki wachache wamewahi kumudu kuifanya
kazi yao kuwa ya muda wote kwa nyakati zote, bila kujali vizazi
vinavyokuja na kupotea, vinavyochagizwa na kukua kwa teknolojia.
Katika kundi la wanamuziki wa aina hiyo, unamkuta Robert Nesta Marley,
ambaye wengi tumezoea kumwita Bob Marley. Ingawa alifariki mwaka 1981,
ndiye mwanamuziki wa Reggae anayefahamika kuliko wengine wote, wakiwemo
wanaoimba hivi sasa!
Wakati Marijani Rajab ‘Jabali la Muziki’ akiimba kibao cha Geogina miaka
mingi iliyopita, hakujua kama leo hii, vijana waliozaliwa miaka ya
themanini na tisini wanacheza na kuimba kibao chake kana kwamba
kimeimbwa na akina Khalid Chokoraa! Hata hivyo, sanaa ya muziki pia
inatambua umahiri wa watu wanaoimba kwa masilahi ya nyakati za kizazi
chao, iwe kwa ajili ya kuiburudisha jamii inayomzunguka, kufundisha,
kuhadharisha na madhumuni mengine kedekede.
Katika kundi hili, kwa wanamuziki wetu wa kizazi kipya, tunao wengi
wanaostahili tuzo. Wanafanya muziki wao kwa faida ya kizazi chao cha
sasa, mashabiki wanapata burudani, wanapewa hadhari, wanafundishwa na
wakati mwingine hata kushauriwa.
Hivi karibuni, Hamis Mwinjuma maarufu kama FA, alisema Rais Magufuli
alimpigia simu na kumweleza kuwa yeye ni shabiki wa muziki wake na kuwa
anakifagilia sana kibao chake kilichopo mtaani kwa sasa, Mwanaume
Suruali! MwanaFA ni mmoja wa marapa wazuri, lakini yeye siyo mkosoaji wa
watawala na wala hajishughulishi na nyimbo zenye mlengo wa siasa,
ingawa ana uelewa wa hali ya juu katika mambo ya siasa kuliko wasanii
wengi.
Kama Rais ameruhusu Wimbo wa Wapo upigwe redioni na tena anaupenda wimbo
wa MwanaFa wa Mwanaume Suruali, Roma amefanya nini? Waliomteka hawawezi
kuwa mawakala wa serikali kwa sababu hatuoni katika wimbo upi watawala
wamekwazika.
Waliomteka hawakuwa na nia ya kumuua, ila kuna kitu tusichokijua
walihitaji kukifahamu kutoka kwake. Kama nilivyosema mwanzo, Roma ni
jasiri. Anajua kama watu hawakutosheka na alichokisema kwenye ile press
conference kwa sababu yule siyo Roma wanayemjua.
Mashabiki wanasubiri Roma awaeleze ukweli kwa sababu hawaamini kama ile ni sinema ya kutafuta kiki.
Hata yeye mwenyewe anajua kama hakuwashibisha. Na bahati mbaya ni kwamba
wote wanajua siku ile hakusema walichotaka kukisikia na
kinachosikitisha zaidi ni kuwa hata akirejea tena na kuongopa, watajua
wamedanganywa.