WAZIRI Mkuu wa zamani wa Israel, Ehud Barak ameipongeza Serikali ya
Tanzania kwa jinsi inavyovitunza vivutio vyake vya utalii. Barak
anayeongoza kundi la watalii zaidi ya 100 kutoka Israel ikiwamo familia
yake, aliwasili nchini mapema wiki iliyopita kwa ajili ya utalii.
Walitembelea Makumbusho ya Olduvai Gorge na kueleza kufurahishwa kwake
na jinsi Serikali inavyofanya katika kuhifadhi maeneo ya kihistoria kama
Olduvai Gorge. Aidha, walitembelea Hifadhi za Taifa za Ngorongoro na
Serengeti zilizoko katika Urithi wa Dunia, unaotambuliwa na Shirika la
Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO).
Meneja Mawasiliano wa Shirika la Taifa la Hifadhi za Taifa (Tanapa),
Pascal Shelutete, alisema Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Israel alizuru
pia Olduvai Gorge akiwa njiani kwenda Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
alikopokelewa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Ramo Makani. Akiwa
Olduvai Gorge ambayo ni moja ya eneo maarufu la masuala la kale katika
Afrika Mashariki na linalotembelewa kwa kiasi kikubwa na watalii
wakienda katika hifadhi za taifa za Ngorongoro na Serengeti, Barak
alisema eneo hilo ni muhimu kutokana na uhusiano wake na binadamu wa
kizazi cha sasa.
Akiwa na msafara wake waliwasili nchini Jumanne iliyopita wakitumia
ndege ya Shirika la Ndege la Israel, na kutua kwenye Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) walipokelewa na Waziri wa Maliasili na
Utalii, Profesa Jumanne Maghembe. Mapema mwezi huu, Balozi wa Israel
nchini, Yahel Vilan alimtembelea Rais John Magufuli na kumueleza kuwa
watalii wapatao 200 walikuwa wanatarajiwa kuitembelea nchi mwezi huu.
Tanzania na Israel zimeapa kudumisha uhusiano wake na ulipata nguvu
zaidi baada ya uamuzi wa Tanzania kufungua ubalozi wake nchini Israel na
kufunguliwa kwa kituo cha Israel cha utoaji viza jijini Dar es Salaam,
Novemba mwaka jana. Sekta ya utalii itanufaika kutokana na hatua hizi.
Kulingana na taarifa za kuaminika kutoka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB),
idadi ya watalii kutoka Israel imeongezeka kutoka 3,007 mwaka 2011 hadi
14,754 mwaka 2015.