Rapa Moni Centrozone amefunguka kwa mara nyingine tena na kudai hawezi kumuonea wivu Roma Mkatoliki kuhusiana na wimbo wake wa Zimbabwe ila wananchi ndiyo wanasababisha mpaka yeye aonekane anachuki na mwenzake.
Moni ameeleza hayo kupitia 'backstage' ya bongo fleva 'top 20' za East Afrika Radio baada ya majuma kadhaa kupita tokea atoe kauli yake mbele ya kamera za eNewz ya EATV ambayo alidai hakufurahishwa na kitendo alichokifanya Roma kutoa wimbo wa Zimbabwe kwa kuita ni usaliti kwa kuwa alijizungumzia yeye binafsi katika wimbo bila ya kuwashirikisha wenzake ambao walitekwa pamoja.
"Hatuna mawasiliano mazuri kati yetu kutokana na maneno ambayo yanaendelea katika jamii, mimi siwezi kumuonea wivu Roma Mkatoliki kwa sababu yeye ameshafanikiwa kimuziki tokea kitambo, nitawaonea wivu wakina Coyo pamoja na Billnass ambao ndiyo kizazi changu kama endapo watafanya vitu vizuri na vikubwa katika maendeleo yao lakini siyo kwa Roma", amesema Moni.
Pamoja na hayo, Moni amedai kitendo cha yeye kuzungumzia wimbo wa Zimbabwe ndicho kinapelekea kuonekana kama anachuki dhidi ya Roma.
"Mimi kuongelea zaidi mambo ya Zimbabwe nimeoneka kama nina 'jelous' na kufanya watu waniongelee vibaya 'so' imekuwa inaleta mtafuruku kwenye jamii, kiukweli sijishughulishi na jambo lolote kuhusiana na Roma kwa sasa", amesisitiza Moni.
Pamoja na hayo, Moni amesema kwa sasa anafanya kazi zake binafsi bila ya kumtegemea msaada wowote kutoka kwa Roma kama ilivyokuwa awali hawajapatwa na tukio la utekwaji na watu wasiojulikana
10 Sept 2017
New