Bulaya Aitupia Lawama Serikali....Adai Imesababisha TANESCO Ifiilisike - MULO ENTERTAINER

Latest

24 May 2018

Bulaya Aitupia Lawama Serikali....Adai Imesababisha TANESCO Ifiilisike

Mbunge Bunda Mjini (Chadema), Ester Bulaya amesema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015 imelifanya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushindwa kujiendesha kwa faida, kutaka ligawanywe.

Bulaya ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Mei 24, 2018 bungeni mjini Dodoma katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati mwaka 2018/19.

Amesema kwa muda mrefu ripoti mbalimbali za kamati za Bunge, ikiwamo ya mashirika ya umma, zinaeleza namna Tanesco inavyojiendesha kwa hasara.

Amesema kabla ya Serikali hiyo haijaingia madarakani, Tanesco ilikuwa ikipata hasara ya Sh124 bilioni lakini baada ya kuingia madarakani Tanesco inapata hasara ya Sh346 bilioni inayotokana na upugufu wa maji na gharama za uendeshaji.

“Tanesco ina madeni ambayo yamepanda kwa asilimia 23. Kabla Serikali hii haijaingia madarakani, Tanesco walikuwa na madeni ya Sh738 bilioni lakini baada ya kuingia yamefikia Sh958 bilioni na haya si maneno ya Bulaya. Ukiangalia ripoti ya CAG, inasema madeni hayana uhusiano kati ya Tanesco na mali, kwa maana nyingine Tanesco imefirisika,” amesema Bulaya.

Amesema wakati madeni haya yanatokea, kulikuwa na ushauri na mikakati mbalimbali ya kuligawanya shirika hilo ili kutenganisha usambazaji na uzalishaji.

“Leo hii tusingekuwa tunazungumza umeme wa vibaba wakati tunataka Tanzania ya viwanda. Wakati haya yanafanyika, Tanesco inashindwa kukusanya madeni makubwa, Tanesco inaidai Hospitali ya Tumaini Dola milioni 9.4 za marekani sawa na Sh18 bilioni na ni kodi ya pango,” amesema.

“Kodi hii ni tangu mwaka 1998 haijawahi kulipwa, kulikuwa na kesi mahakamani na Tanesco ikashinda na mahakama imeitaka kuondoka lakini mpaka sasa haijachukua hatua zozote.”

Mbunge huyo pia alihoji kitengo cha wizara hiyo kutenga Sh700 bilioni kwa ajili ya mradi wa umeme wa Stiegler’s Gorge badala ya fedha hizo kuzipeleka Rea (Wakala wa Umeme Vijijini) na Tanesco.

“Mkiona wengine tunasema hivi mjue yametuchosha timizeni wajibu wenu acheni mbwembwe ndogondogo,”amesema.