Hii ndio sababu ya mabadiliko kesi kina Malinzi - MULO ENTERTAINER

Latest

29 May 2018

Hii ndio sababu ya mabadiliko kesi kina Malinzi

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana iliahirisha usikilizaji ushahidi wa Jamhuri katika kesi ya kutakatisha Dola za Marekani 173,335 (Sh. milioni 43.1) inayowakabili vigogo wa Shirikisho la Soka (TFF).

akiwamo rais wa zamani Jamali Malinzi, hadi Juni 11 kwa sababu hakimu anayesikiliza kesi hiyo amepata udhuru wa kikazi.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa ushahidi jana na leo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri.

Hata hivyo, ilitajwa mbele ya Hakimu Mkazi Martha Mpanze baada ya Hakimu Mashauri kuwa na udhuru wa kikazi.

Mbali na Malinzi, washitakiwa wengine ni katibu mkuu, Selestine Mwesigwa, mhasibu Nsinde Mwanga, meneja Miriam Zayumba na karani Flora Rauya, wote wa TFF.

Wiki iliyopita, shahidi wa kwanza wa Jamhuri katika kesi hiyo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi ya TFF, Boniface Wambura alidai haufahamu muhtasari wa kikao cha kamati ya utendaji iliyopitisha mabadiliko ya watia saini wa TFF wa Juni 5, 2016.

Alidai kwamba muhtasari huo ambao umetiwa saini na mwenyekiti wa kamati hiyo, rais Malinzi na katibu Selestine Mwesigwa ulikuwa wa kughushi.

Shahidi huyo alidai anakumbuka katika kikao hicho ambacho naye alikuwa mjumbe, hakukuwa na ajenda ya kubadilisha mtia saini kutoka Edgar Masoud kwenda Nsiande Mwanga, Alidai kuwa muhtasari ulioorodheshwa majina yao wa Juni 15, 2016 ni wa kughushi na haufahamu.

Alidai kuwa mchakato wa kubadilisha watia saini unatakiwa kupitia katika kamati ya utendaji ukieleza kufanya mabadiliko, na kamati hiyo ikiridhia mabadiliko hufanyika na kikao kinachofuata hupitisha.

KULA NJAMA
Katika kesi hiyo, Malinzi anakabiliwa na mashtaka 28 ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa Dola za Kimarekani 173,335 na Sh. 43,100,000.

Katika hati hiyo, Mwesigwa anakabiliwa na mashtaka sita ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi na utakatishaji fedha.

Kadhalika, Mwanga anakabiliwa na mashtaka mawili ya utakatishaji fedha wakati Zayumba anakabiliwa na mashtaka tisa ya kughushi huku Rauya akikabiliwa  na shtaka moja la kughushi.

Katika maelezo ya awali washtakiwa wote walikiri anuani zao, nafasi zao za kazi lakini kukana kutenda makosa yote yanayowakabili.

Katika maelezo hayo ilidaiwa TFF inamiliki akaunti sita katika benki ya Stanbic na kwamba mtia saini wa akaunti hizo alikuwa ni Edgar Masoud.

Ilidaiwa kuwa Septemba Mosi, 2016 mshtakiwa wa pili aliwasilisha maamuzi ya kamati tendaji ya TFF katika benki ya Stanbic ambayo yalionesha TFF imemuondoa Edger kuwa mtia saini wa akaunti hizo na kuwa Nsiande; ambapo mabadiliko hayo yalikuwa yameghushiwa na Malinzi na Mwesigwa.

Ilidaiwa kuwa baada ya Mwesigwa kumtambulisha Nsiande kuwa mtia saini katika akaunti hizo za TFF, alihusika kutia saini katika nyaraka za malipo kati ya Juni Mosi na Desemba 31, 2016.

Upande huo wa Jamhuri ulidai kuwa washtakiwa  Zayumba na Flora ndiyo waliokuwa wakiziandaa risiti bila ya kujali kuwa hawakuwa wakipokea fedha kutoka kwa Malinzi.

Kimaro alidai kuwa Mwesigwa kwa nafasi yake alihusika kikamilifu kuhakikisha Malinzi analipwa na Nsiande alihusika kusaini nyaraka za malipo Juni Mosi hadi Desemba 31, 2016 ambapo Malinzi alilipwa jumla ya dola za Kimarekani 173,335 na Sh. milioni 40.1.

Kutokana na hayo yote, washtakiwa hao walikamatwa, wakahojiwa na kufikishwa mahakamani hapo.