Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema amefunguka kuwa bado wanaendelea kutafakari suala la Mbunge wa Sigida Mashariki Tundu Lissu kuhangaika na kutafuta misaada ya matibabu kwa watu mbalimbali duniani, kwani Bunge bado linatafakari kuhusu stahiki zake, haki na gharama za matibabu.
Mhe. Lema amezungumzia hayo ikiwa ni siku moja tangu kutokea kwa kifo cha Mbunge wa Buyungu, Kasuku Bilago aliyefariki wakati akipatiawa matibabu katika hospitali ya Taifa, Muhimbili.
Lema amesema "Mwili wa Marehemu Mhe. Bilago umepata heshima, haki na stahiki ya Kibunge, tumefanya kikao tena Kati ya Bunge, Chama na Familia, wema wa Bunge kwa mwili wa marehemu umekuwa ni wa kifani".
Ameongeza "Wakati tunalishukuru Bunge kwa wema huu, bado tunaendelea kulitafakari la rafiki yetu Lissu aliyeko Ubeligiji".
Lissu ambaye anatibiwa nchini Ubelgiji alipigwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 9, 2017 maeneo ya Area D akiwa anatokea katika majukumu yake ya kikazi bungeni Dodoma.
Sababu za Lissu kutotibiwa na Bunge ziliwekwa wazi na Spika wa Bunge, Job Ndugai siku moja baada ya tukio hilo ambapo alisema kuwa utaratibu wa matibabu kwa mbunge ulikuwa umeshafuatwa lakini familia pamoja na chama waliamua kumpeleka Nairobi, na siyo kama wao walishindwa kumpeleka nchini India.
28 May 2018
New