Nora wa Bongo Movies Aamua Kujivua..."Kazi Niliyotumwa na Mungu Nimeimaliza" - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Sept 2018

Nora wa Bongo Movies Aamua Kujivua..."Kazi Niliyotumwa na Mungu Nimeimaliza"


Msanii wa filamu nchini, Nuru Nassoro maarufu kama Nora ametangaza rasmi kuachana na masuala ya sanaa ya uigizaji, huku akidai hata ikitokea amefariki hii leo atajisikia furaha kwa kuwa kazi iliyomleta duniani ameikamilisha.

Nora ameeleza hayo kupitia ukurasa wake wa kijamii wa Instagram huku akiwakosoa baadhi ya wasanii wa sasa wa filamu kuwa wamejawa na utandawazi, jambo ambalo linawapelekea kufanya mambo yasiyokuwa na maadili kwenye mitandao ili kusudi wapate kusifiwa, kujulikana na kupendwa.

"Nimeacha historia kwenye maisha yenu, kila mnapo nikumbuka kumbukumbu nzuri za furaha zinawajia kwenye vichwa vyenu, mpaka mnatamani enzi hizo zingekua zinarudi. Namshukuru MUNGU wangu sana kwa hili kwani ni kitu kizuri ukifanya kitu na watu wakakukumbuka kwa mazuri kiukweli ninapata furaha mnoo, ambayo haielezeki...

Japo najikuta najisikia vibaya wengine wanaposema walikua wanafukuzwa kwenye 'sitting room' za watu lakini ilibidi wakae madirishani na ikibidi wakate madirisha ya watu, wengine walikua wanakalishwa chini au inawabidi wafanye kazi ili jioni inapofika waangalie kipindi. Ninawatangazia rasmi nimeacha kuigiza.", ameandika Nora.

Pamoja na hayo, Nora ameendelea kwa kusema kuwa "mapenzi yenu yalikuwa sio ya kawaida wallah, hata nikifa leo kazi ilio nileta duniani ya kuwa burudisha na kuwafundisha nilifanya kwa ufasaha. Ama kweli enzi haziwezi kurudi, sasa hivi dunia imekua ya utandawazi watu wamekuwa wakilazimisha kupendwa, kusifiwa, kujulikana, inafikia wakati maadili hamna, mazoea ya kukaa pamoja kama familia na kuburudika na kujifunza".

Mbali na hilo, Nora amesema kuwa anajivunia kuwa msanii wa zama za zamani kuliko sasa, kwa kile alichokidai kwamba kizazi hiki kimeharibiwa na utandawazi katika kila kona.

"Nimeacha alama ambayo haitofutika daima niko hai au nimekufa, alama ambayo hata kwa Mungu ninacho cha kujitetea na akanielewa kwa kuwa siku lazimisha umaarufu ulikuja wenyewe, sikudanganyika na dunia bali niliishi kadri umri ulivyo nihitaji. Mara zote niliipigania heshima yangu kwenye kila kitu kama binadamu nilikosea lakini sio kwa makusudi eti ili niitawale dunia", amesisitiza Nora.

Nora alianza kujipatia umaarufu kwa jamii kupitia 'Kaole Sanaa Group', ambao walikuwa wanafanya maigizo yaliyokuwa yanayoeneshwa katika televisheni ya ITV.

Nora ni miongoni mwa wasanii waliowahi kuigiza na marehemu Steven Kanumba katika filamu ya 'Dangerous Desire' ambayo alivaa uhusika wa mke wa Kanumba.