Serikali Imefuta Tozo za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi - MULO ENTERTAINER

Latest

20 Sept 2018

Serikali Imefuta Tozo za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi

Serikali Imefuta Tozo za Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi
Serikali imefuta tozo tano zilizokuwa zikitozwa na Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA ) lengo likiwa ni kuwapunguzia mzigo waajiri.

Tozo zilizofutwa ni ada ya fomu Shilingi 2,000 , ada ya ukubwa wa eneo la kazi ambayo ilikuwa ni kati ya Shilingi 50,000 hadi Shilingi milioni 1.8. Nyingine ni ada ya leseni na ada ya ukaguzi Shilingi 200,000 ada ya vifaa vya kuzimia moto Shilingi 500,000 na siku ya usalama kazini ambayo ilikuwa ikitozwa Shilingi 450,000.

Akitangaza kufutwa kwa tozo hizo leo Alhamisi Septemba 20, 2018 wakati akizungumza na wanahabari Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama amesema kuondolewa kwa tozo hizo ni agizo la Rais John Magufuli, ambapo amesema OSHA, imepitia mambo mengi ikiwemo kupunguza ratiba za ukaguzi ambazo zimekuwa zikifanyika mara kwa mara hasa katika sekta binafsi.

“Kwa mfano katika sekta binafsi kulikuwa na maumivu makubwa zaidi, yaani huyu anakagua hili, kesho mwingine, keshokutwa tena, sasa haipo hiyo na badala yake vyote vitakaguliwa kwa wakati mmoja, kwani tuna mfumo wa taasisi zote kwenda pamoja”, amesema Mhagama.

Amesema utekelezaji wa punguzo la tozo hizo umeanza mara moja kuanzia yalipoanza mabadiliko ya fedha mwaka wa fedha hivyo akatoa onyo kwa watumishi watakaojihusisha na utozaji wa tozo hizo.

Takwimu zinaonyesha kuwa jumla ya ajali 755 ziliripotiwa mahali pa kazi na kati ya hizo vifo vilikuwa 6 na 749 ni majeruhi huku sekta ya uzalishaji iliongoza kwa asilimia 87, madini asilimia 7, ujenzi asilimia 4 na sekta nyingine asilimia 2.