Waziri Mkuu Atangaza Kiama Kwa Majambazi, Watekaji Watoto - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Feb 2019

Waziri Mkuu Atangaza Kiama Kwa Majambazi, Watekaji Watoto


Waziri  Mkuu, Kassim Majaliwa ametangaza vita na watu wanaoteka watoto na kudai fedha na wakati mwingine kuwaua watoto hao.

Akizungumza katika kikao na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Kigoma alipoanza ziara ya siku nne mkoani humo jana, Majaliwa amesema ameamua kulivalia njuga suala hilo na masuala ya ujambazi ambayo kwa kiasi kikubwa yanafanywa na wageni kutoka nje wilaya Kibondo na Kakonko.

Katika kuhakikisha anaanza utekelezaji kwa vitendo wa suala hilo, anafanya ziara yake mkoani Kigoma kwa njia ya barabara ambako atapitia maeneo yenye matatzo hayo akienda mkoani Kagera.

Waziri Mkuu alisema pamoja na utekaji wa watoto matumizi ya silaha, pia ni makubwa katika maeneo hayo hivyo anaanza mkakati wake kwa kuzungumza na wakimbizi wa Burundi katika kambi ya Nduta Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma na kwamba vitendo hivyo lazima vikomeshwe.

Akizungumzia kilimo cha michikichi, alisema serikali imeamua Kigoma kuwa mkoa kiongozi katika kilimo cha michikichi na ziara yake inafuatilia maagizo yaliyotolewa katika utekelezaji wa mikakati mbali mbali ya kuinua zao hilo.

“Niliagiza kuwepo chuo kwa ajili ya uzalishaji mbegu naambiwa kimeshaanza sambamba na vitalu vya miche, upanuzi wa mashamba na kuhakikisha maeneo ya uzalishajii wa zao hilo yapo ya kutosha,” amesema Waziri Mkuu.

Amesema Serikali pia inataka kuvutia wawekezaji wakubwa katika zao hilo, lakini pia kuona wakulima wadogo wanapewa nafasi kushiriki kwenye kilimo cha zao hilo na wanapewa maeneo ya uzalishaji.