Jorge Mendes wakala wa kipa namba moja wa Manchester United David de Gea, amewatoa shaka mashabiki wa klabu hiyo kwa kuwaambia kuwa mteja wake haondoki Old Trafford.
Kipa huyo ambaye mkataba wake wa sasa utafikia ukingoni mwishoni mwa msimu ujao, amekuwa akihusishwa kwa kiasi kikubwa na uhamisho wa kwenda Real Madrid.
Lakini Jorge Mendes amesema anaamini kipa huyo mwenye kipaji cha hali ya juu atabakia Old Trafford.
“Amebakiza mwaka mmoja wa mkataba wake lakini naamini atabakia Manchester United,” Mendes aliiambia BBC. “Mchezaji ataamua mwenyewe lakini ana furaha kuwa pale.”
Maoni ya Mendes yanakuwa ni nafuu kwa mashabiki wa Manchester United ambao walianza kuamini kuwa kipa huyo aliyesajiliwa kwa pauni milioni 17.8 mwaka 2011, yuko njiani kuondoka.
Wiki iliyopita kocha wa United Louis van Gaal alipoulizwa kuhusu hatma ya kipa huyo alikiri kuwa lolote linawezekana.