UKAWA ipo Imara Sana Kuliko Kawauda Lazima itachukua Nchi- Ester Bulaya - MULO ENTERTAINER

Latest

5 Aug 2015

UKAWA ipo Imara Sana Kuliko Kawauda Lazima itachukua Nchi- Ester Bulaya

Aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu wa CCM aliyehamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Ester Bulaya amefunguka na kusema kuwa

Umoja ya Katiba ya Wananchi (UKAWA) upo imara na utachukua dola japo amekiri kunachangamoto mbalimbali kutoka kwa chama tawala kutaka kuvuruga umoja huo.
Ester Bulaya ameyasema haya leo alipokuwa aki-chat live katika ukurasa wa facebook wa EATV katika Kipengele cha Kikaangoni ambacho huwa kinawakutanisha wananchi na watu mashughuri kila siku ya Jumatano kuanzia saa nane mchana mpaka kumi alasiri.

Katika zoezi hilo watu wengi walitaka kujua iwapo UKAWA unaweza kuchukua nchi na kukishinda Chama cha Mapinduzi (CCM) ndipo Ester Bulaya alipotoa mtazamo wake juu ya umoja huo ambao anadai ni tishio kubwa kwa CCM hivi sasa.
"Ukawa upo imara na utachukua nchi, ingawa changamoto hazikosekani pale ambapo mafanikio yapo karibu, kwani dola imejitahidi kuhakikisha Ukawa unasambaratika lakini kwa nguvu za Mungu bado umoja huo umesimama imara," alisema Ester Bulaya

Licha ya hayo Ester Bulaya aliweza kuweka wazi kilichomsukuma kukihama CCM na kwenda Chadema na kudai aliamua kufanya maamuzi hayo magumu kwa kuwa anachokiamini yeye na kukisimamia ni sawa na misingi na itikadi za Chadema, hivyo kutokana na maamuzi yake hayo anaamini yupo sehemu sahihi na yupo huru. Bulaya pia amedai misimamo yake pamoja na anachokiamini kilikuwa kinawakwaza CCM.

"Niliziona kasoro baada ya kuwa mbunge wa viti Maalum (CCM), kwani nikiwa umoja wa vijana ndani ya CCM moja ya mambo mnayofundishwa kwamba vijana ni watetezi wa taifa hili na sauti ya chama na kukemea maovu, nilipo anza kufanya vile nilivyofundishwa ikaonekana ni tatizo, hivyo nikagundua CCM inahubiri vitu tofauti na inavyoviamini, mdomoni unapaswa kusema vingine moyoni uamini vingine," alifafanua Ester Bulaya.
Katika hataua nyingine Ester Bulaya amedai kujifunza mambo mengi ndani ya muda mfupi alipohamia Chadema, kwani amegundua wazi kuwa viongozi na wananchama wake wapo tayari kujitolea kujenga na kuleta mabadiliko kwa watanzania.

"Kila chama kina utaratibu wake, lakini nilichojifunza Chadema viongozi na wanachama wake wapo tayari kujitolea kujenga chama na kuleta ukombozi wa kweli kwa watanzania na pia Chadema wanachokiubiri na kukiamini ndicho wanachokisimamia," alisema Ester Bulaya.

Amesema malengo yake ndani ya chadema ni kuungana na jeshi la ukombozi kuleta mageuzi ya kweli, siasa safi za demokrasia ya kweli na kuwakomboa watanzania kwa kuwaletea maendeleo ya kweli kutokana na rasilimali zao ambazo kwa miaka 50 ya utawala wa CCM wameshindwa kuyapata.
Ester Bulaya alikuwa mbunge wa kwanza kutoka katika Chama Cha Mapinduzi na kuhamia Chadema pamoja na aliyekuwa mbunge wa jimbo la Kahama James Lembeli ambao walitambulishwa na kukabidhiwa kadi za Chadema katika mkutano wa Chadema uliofanyika Jijini Mwanza.