Nape Toa Mpya..Aitaka Chadema Kumfukuza Edward Lowassa - MULO ENTERTAINER

Latest

14 Jan 2016

Nape Toa Mpya..Aitaka Chadema Kumfukuza Edward Lowassa

CCM imemjibu mwanasheria Mkuu wa Chadema ikisema ili chama hicho kikuu cha upinzani kionekane kinapambana na ufisadi kwa vitendo, kinatakiwa kumuunga mkono Rais John Magufuli na kumvua uanachama Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho tawala, Nape Nnauye alisema Chadema iliachana na ajenda ya kupambana na ufisadi baada ya kumpokea Lowassa  Julai mwaka jana baada ya jina lake kukatwa katika mchakato wa CCM kusaka mgombea wake wa urais.
“Sisi hatukumpitisha (Lowassa) awe mgombea wetu wa urais kwa sababu hiyo (ya ufisadi) na ndiyo maana yeye mwenyewe aliamua kuondoka na kwenda Chadema,” alisema Nape.
“Hata katika kampeni za uchaguzi mkuu, Chadema hawakuzungumzia ajenda ya ufisadi, ni kama Lowassa aliifunika tu.”
Alikuwa akimjibu Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu ambaye  juzi alisema ufisadi ni ajenda ya kudumu ya chama hicho kwa kuwa Rais Magufuli hataweza kuufumua wote katika kipindi cha miaka mitano.
Huku akichelea kueleza kiundani sababu za CCM kutomfukuza Lowassa kwa tuhuma za ufisadi mpaka alipoamua kujiondoa na kujiunga na Chadema, alisema kauli ya Lissu inalenga kuwahadaa Watanzania.
“Kauli ya Lissu ni ya kushangaza sana. Sisi tunajua jinsi ambavyo Chadema na washirika wake walivyojitenga na ajenda ya ufisadi. Kama kweli wanaupinga, basi wamuunge mkono Rais Magufuli ambaye kwa sasa anapambana na ufisadi kwa kasi,” alisema mbunge huyo wa Mchinga.
“Wakati mwingine kila jambo hufanyika kwa wakati wake. Suala la kupinga ufisadi CCM lilianza siku nyingi tangu enzi za kujivua gamba. Tumeendelea nalo mpaka watu wakajiondoa wenyewe,” alisema Nape.
Alisema hoja ya kupinga ufisadi ndani ya CCM ilikibeba chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kikapata ushindi mnono, huku Chadema iliyokuwa ikilia na ufisadi ikishindwa.
 “CCM tulieleza sababu za kutompitisha Lowassa kugombea urais na hilo lilikuwa wazi,” alisema.
Katika ufafanuzi wake wa juzi, Lissu alisema ili apambane na ufisadi, Rais Magufuli anapaswa kuacha tabia za CCM na kumtaka mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) amtangaze mshindi halali wa Uchaguzi Mkuu ambao Chadema wanaamini Maalim Seif Sharif Hamad alishinda.
Pia Lissu alimtaka Rais ataje majina ya waliokwepa kodi ili kama watajitokeza kuwania uongozi, wadhibitiwe kwa kuwa Katiba imezungumza kwa maneno makali dhidi ya vitendo hivyo viovu.
Aidha, aliponda uteuzi wa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo anayetajwa kuhusiska katika sakata la uchotwaji wa Sh3060 bilioni kutoka akaunti ya Tetega Escrow.
Miaka 39 ya CCM
Akizungumzia maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 39 ya kuzaliwa kwa CCM, Nnauye alisema uzinduzi utafanyika Januari 31, visiwani Zanzibar na mgeni rasmi atakuwa makamu mwenyekiti wa chama hicho na Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.
Alisema kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Februari 6, mjini Singida na yataongozwa na mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye aliiongoza Serikali ya Awamu ya Nne.
“Viongozi wa kitaifa na baadhi ya wajumbe wa Kamati Kuu watakaohudhuria maadhimisho haya watapangiwa shughuli za ujenzi wa chama na taifa katika wilaya zote za mkoa wa Singida, siku tatu kabla ya kilele cha maadhimisho,” alisema.
Alisema mikoa yote nchini inapaswa kuandaa shughuli hiyo wiki moja kabla ya maadhimisho, na kwamba lengo ni kufanya shughuli za ujenzi wa chama hicho katika maeneo yao.
“Tutakachokifanya wiki hiyo ni kupokea wanachama wapya, kufanya mikutano ya kuwashukuru wananchi kwa kuiamini CCM na kuichagua iendelee kuongoza, kuhamasisha wananchi kufanya kazi ili kujiletea maendeleo,” alisema.