Sakata la Rushwa Kamati za Bunge..Zitto Kabwe Aitwa na Takururu Kuhojiwa..Mwenyewe Asema Haya - MULO ENTERTAINER

Latest

25 Mar 2016

Sakata la Rushwa Kamati za Bunge..Zitto Kabwe Aitwa na Takururu Kuhojiwa..Mwenyewe Asema Haya

Siku tatu baada ya kuibuka kwa kashfa ya rushwa miongoni mwa wajumbe wa Kamati za Kudumu za Bunge, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imemuita Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kumhoji.

Muda mfupi baada ya taarifa za kashfa hiyo kuwa wazi, Zitto na mwenzake wa Nzega Mjini, Hussein Bashe ambao ni wajumbe wa Kamati ya Huduma za Jamii, walimuandikia barua Spika wa Bunge, Job Ndugai kujiondoa kwenye nafasi zao ili kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma hizo.

Zitto alithibitisha kupata wito kutoka makao makuu ya Takukuru ili kuhojiwa juu ya sakata hilo na akapongeza kuwa endapo vyombo vya Serikali vitakuwa makini kushughulikia tuhuma zote zinazoelekezwa kwa wanasiasa na watumishi wengine wa umma, itasaidia kuongeza uwajibikaji na kupunguza uzushi kwa wananchi.

“Nimepata wito huo kupitia Ofisi ya Bunge. Nasikia Bashe ameitwa pia. Nafurahi wito wetu wa uchunguzi umechukuliwa kwa uzito unaostahili na tutatoa ushirikiano wote kwa vyombo vya uchunguzi ili kumaliza zoezi hili kwa haraka na kwa ufanisi,” alisema Zitto.