Waziri wa Mambo ya Nje nchini Marekani John Kerry akiwa na mshindi wa tuzo ya Mwanamke Jasiri wa Kimataifa Bi.Vicky Ntetema
Serikali ya Marekani imemtunuku Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali Under the Same Sun Tanzania, Vicky Ntetema tuzo ya ‘Mwanamke Jasiri wa Kimataifa’, ‘International Women of Courage.’
Ntentema alikabidhiwa tuzo hiyo jana nchini Marekani na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, John Kerry jijini Washington DC.
Kupitia taasisi hiyo Ntetema ambae pia aliwahi kuwa mtangazaji wa BBC, amekuwa akitetea haki za watu wenye ulemavu wa ngozi yaani (Albino)nchini Tanzania, kupigania haki zao, kupinga matendo ya kikatili yanayofanywa dhidi yao kama kubaguliwa na kukatwa kwa viungo vyao kutokana na imani za kishirikina.
Ni mmoja kati ya wanawake watatu ambao wametunukiwa tuzo hiyo, wengine wakitokea Sudan na Mauritania.
Tuzo hizi zilianza kutolewa rasmi tangu mwaka 2007 ambapo hadi sasa wanawake takriban 100 kutoka kwenye nchi zaidi ya 60 wameshajizolea tuzo hizo za heshima.
Tuzo hizi hutolewa kila mwaka kwa wanawake duniani ambao wameweza kuonyesha ujasiri katika kupigania haki za wanyonge, amani, usawa wa kijinsia.
Taarifa kwa umma iliyotolewa na ofisi ya Waziri wa Masuala ya Nje Marekani Bw. Kerry imempongeza Bi. Ntetema na kuongeza kuwa Mwanamama huyo ametumia muda wake mwingi mafichoni kukutana na waganga wa jadi/kienyeji akikusanya ushahidi na taarifa kuhusiana na ongezeko la mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi Albino na uuzwaji wa viungo vyao.