MSANII anayefanya muziki na filamu Bongo, Sabrina Omary ‘Sabby Angel’ amefunguka kwa kinywa chake kuwa penzi la mwanamuziki mkali wa Bongo Fleva, Ali Salehe Kiba ‘Alikiba’ lilitaka kutoa uhai wake kwani hakuna mwanaume aliyemshika mtima wake zaidi yake.
Akizungumza na gazeti hili juzikati, Sabby anayedai ana historia ya kutendwa na wanaume alisema kuwa amewahi ‘kudate’ na wanaume wapatao saba lakini kati yao hakuna aliyemdatisha zaidi ya Kiba ila jamaa huyo alitaka kusababisha ajitoe uhai.
“Jamani haya mapenzi yaacheni hivihivi, huwezi kuamini Alikiba alitaka kuniua kwa penzi lake, nilimpenda sana na alinidatisha kiasi kwamba nilipokuwa nikihisi ananisaliti, niliumia roho na wakati mwingine kupata presha.
“Achilia mbali hilo, kuna wakati nilitaka kujiua kwa sababu yake maana kuna kitu kilitokea, nikaumia sana hadi nikahisi sina umuhimu wa kuishi,” alisema mdada huyo.
Inadaiwa Sabby na Kiba waliwahi kuwa wapenzi kwa siri na haikuchukua muda mrefu wakamwagana kwa sababu ambazo wanazijua wenyewe.
Ijumaa lilifanya jitihada za kumtafuta Kiba angalau agusie kidogo uhusiano wake na binti huyo ulivyokuwa lakini hakuweza kupatikana mara moja.