CHAMA cha ACT-Wazalendo kimesema kinaunga mkono kazi zinazofanywa na Rais John Magufuli pamoja na serikali yake kwa sababu kuna mambo mazuri yanafanyika.
Akihutubia katika mkutano wa kampeni za udiwani jana, katika kata ya Kijichi Dar es Salaam, Kiongozi wa chama hicho, Kabwe Zitto alisema hawajutii kumuunga mkono Rais Magufuli.
Katika mkutano huo, Zitto amewaomba pia wananchi wa Kijichi kumchagua mgombea udiwani wa chama hicho, Edgar Mkosamali katika uchaguzi utakaofanyika Januari 22 mwaka huu.
“Sisi kama chama, ACT Wazalendo tulimuunga mkono Rais tangu mwanzo wa utawala wake na kumkabidhi Ilani ya uchaguzi ya chama chetu kama ishara ya kwamba uchaguzi umekwisha na sasa tujenge nchi yetu. Hatujutii kumuunga mkono kwa sababu kuna mambo mazuri amefanya kuhusu nchi yetu,” alisema Zitto.
Zitto alizitaja kazi ambazo chama chake kinaunga mkono rais kuwa ni pamoja na kupambana na rushwa na ufisadi nchini.
“Ameondoa hali ya ‘impunity’ iliyokuwa imeshika mizizi nchini na kuwawajibisha watendaji na waziri aliyekiuka maadili ya kazi”.
Hata hivyo, Zitto alisema chama chake kinamuomba Rais Magufuli na serikali yake kuwa wasikivu katika matatizo yanayowakumba watanzania, ikiwa ni pamoja na upugufu wa chakula nchini jambo ambalo hivi karibuni alilizungumza na kusema kuwa nchi haina njaa na kwamba hayuko tayari kugawa chakula.