KAMA kuna waziri au kiongozi yeyote anataka kutoa taarifa yenye kuwagusa
wananchi moja kwa moja, ni dhahiri kuwa sasa atalazimika kujiridhisha
zaidi.
Aidha, waziri na viongozi wengine wanatakiwa pia kuzingatia dhana ya
uongozi wa pamoja kwa kuwahusisha wenzao na pia kupata maoni ya
wataalamu katika wizara au taasisi wanazoziongoza kabla ya kulifikisha
kwa umma.
Vinginevyo, mawaziri wajiandae kushuhudia maagizo yao yakitenguliwa huku
pia wakijiweka katika hatari ya kufikiriwa kuwa wanafanya hivyo kwa
minajili ya kutumia matamko yao kama ‘kiki’ za kuwaonyesha kuwa
wanafanya kazi vyema na kwa kasi inayosisitizwa na Serikali ya awamu ya
tano.
Angalizo hilo limetolewa na baadhi ya wachambuzi wa amsuala ya kisiasa
walizoungumza na Nipashe kuelezea mkasa uliomkuta Waziri wa Sheria na
Katiba, Dk. Harrison Mwakyembe, ambaye agizo lake la kuzuia ufungishaji
ndoa kwa watu wote wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa lilifutwa na Rais
John Magufuli kwa kuonekana kuwa litawaathiri mamilioni ya Watanzania
wasiokuwa na vyeti hivyo.
Baadhi ya wachambuzi walidai kuwa Mwakyembe siyo waziri au kiongozi wa
kwanza kutoa taarifa zilizomlazimu Rais Magufuli kuingilia kati kwa
manufaa ya Watanzania na hivyo, wanapaswa kujua kuwa wana wajibu mkubwa
kwa taifa na kutakiwa wajiepushe na matamko binafsi yasiyofanyiwa kazi
kwa kina kabla ya kutolewa kwa umma.
“Ni vizuri kwa kila waziri au kiongozi yeyote yule kujipa uhakika wa
kila tamko na amri wanazotaka kutoa kwa umma…kwa mfano, ni lazima
wahakikishe kwamba wanazingatia sheria na pia wanayoyasema ni kwa
maslahi ya umma mpana wa Tanzania.
“Vinginevyo, matamko yao yataendelea kuibua maswali na Rais hatakubali
wamharibie kwa sababu ameshasema mara kadhaa kuwa daima atakuwa upande
wenye maslahi kwa wananchi wake, na hasa wanyonge,” alisema mmoja wa
wachambuzi hao.
“Ni vizuri wakaachana na matamko yenye viashiria vya kuwa na kiki za
kuonyesha kuwa nao wako vizuri kuendana na kasi ya serikali ya
sasa...wasipozingatia hayo kila mara watajikuta wakiwa tofauti,”
mwingine aliongeza.
Neno ‘kiki’ ni la mtaani na limejitwalia umaarufu katika siku za hivi
karibuni, likitumiwa kumaanisha mbinu zinazoweza kutumiwa na mtu ili
kujipatia umaarufu juu ya jambo fulani. Wasanii na wanasiasa huhusishwa
zaidi na neno hilo kutokana na asili ya kazi zao ambazo huwakutanisha
zaidi na watu.
Awali, katika agizo lake hilo ambalo alilisisitiza pia jana asubuhi
wakati akizungumza na kituo kimoja cha redio jijini Dar es Salaam,
Mwakyembe alisema wameamua kuzuia ndoa kwa watu wasiokuwa na vyeti vya
kuzaliwa kwa nia ya kuondokana na takwimu za sasa zinazoonyesha kuwa
Tanzania Bara ni ya mwisho barani kwa utoaji wa vyeti vya kuzaliwa kwa
wananchi wake.
Alisema ni asilimia 12 tu ya Watanzania walioko Bara ndiyo wenye vyeti
vya kuzaliwa na kuzidiwa hata na Zanzibar yenye wastani wa asilimia 75,
hali aliyosema inashangaza kwa sababu bei ya vyeti hivyo ni Sh. 3,500 tu
huku gharama za harusi zikiwa kubwa kulinganisha na kiasi hicho.
Hata hivyo, akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi kabla ya
kuondoka mjini Dodoma na baadaye taarifa yake kusambazwa kwa umma jana,
Rais Magufuli alisema anatengua uamuzi huo wa Waziri Mwakyembe kwa
sababu utawanyima fursa ya kuoana Watanzania ambao wengi wao hawana
vyeti hivyo vya kuzaliwa, hasa wale wa vijijini.
Alisema hadi sasa idadi ya Watanzania walio na vyeti vya kuzaliwa ni
chini ya asilimia 20 huku wengi wao wakiwa ni wananchi waishio vijijini
ambako ni vigumu kupata vyeti hivyo, na wengine wakiwa ni waliozaliwa
kabla ya kuanza kutolewa kwa vyeti vya kuzaliwa nchini mwaka 1961.
“Kwa hiyo ndugu zangu Watanzania msiwe na wasiwasi wowote, endeleeni na
utaratibu wenu wa kuoa na kuolewa kama kawaida na kama kuna kifungu
chochote cha sheria kinachomlazimisha mtu awe na cheti cha kuzaliwa
ndipo aoe ama aolewe nitamuelekeza Waziri wa Katiba na Sheria Mhe.
Harrison Mwakyembe apeleke Bungeni kikarekebishwe” alisema Rais
Magufuli, huku akitoa wito kwa wanasheria kuziangalia vizuri sheria
zinazohusiana na kuzaliwa na kifo na kuoa na kuolewa ili zisilete
mkanganyiko kwa wananchi.
JPM ALIVYOZIMA ‘KIKI’
Mbali na tukio la kuzimwa kwa ‘kiki’ ya Waziri Mwkayembe jana, wapo pia
mawaziri na viongozi wengine kadhaa wa serikali na taasisi za umma
waliokumbana na rungu la Magufuli la kutengua amri au tarifa zao. Hao ni
pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi,
Vijana, Ajira na Walemavu, Jenista Mhagama; Waziri wa Nchi Ofisi ya
Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George
Simbachawene na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape
Nnauye.
Mhagama alikumbana na mkasa huo Machi 3, 2016 wakati alipotoa taarifa ya
kumteua Dk. Carina Wangwe kuwa Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Taifa la
Hifadhi ya Jamii (NSSF). Hata hivyo, wakati uamuzi wake ukimpa umaarufu
siku hiyo kupitia ‘kiki’ za kwenye mitandao ya kijamii, waziri huyo
alilazimika kubatilisha taarifa hiyo kabla Rais Magufuli hajamtangaza
Prof. Godius Kahyarara kushika nafasi hiyo NSSF.
Agosti 12 mwaka jana, Simbachwene alisisitiza kuondolewa kwa wamachinga
maeneo ya mijini. Hata hivyo, siku chache baadaye, Magufuli alitengua
agizo hilo wakati akihutubia jijini Mwanza kwa kutaka wamachinga
wasiondolewe kwenye maeneo wanayofanyia biashara hadi pale mamlaka
husika zitakapohakikisha kuwa zimewatafutia sehemu za kwenda kufanyia
biashara zao.
Waziri mwingine aliyekumbwa na rungu la Magufuli hivi karibuni wakati
kauli yake ikiwa imepamba moto na kuibua mijadala kwenye mitandao ya
kijamii ni Nape.
Machi Mosi mwaka huu, Nape alielezea umuhimu wa kulinda majina ya
wasanii waliotajwa hadharani wakituhumiwa kuhusika na dawa za kulevya,
akisema kwamba ni vyema kuzingatia nguvu kubwa walizotumia kujijengea
majina hayo na kwamba, ifikiriwe pia ni kwa namna gani watasafishwa
ikiwa wataonekana baadaye kuwa hawahusiki na dawa za kulevya.
Nape alizungumza hayo akiwa Dodoma na baadaye kwenye kipindi cha Dakika
45 kinachorushwa na ITV kuelezea hatua iliyochukuliwa na Mkuu wa Mkoa wa
Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyetangaza hadharani majina ya wasanii
kadhaa katika orodha yake ya awali ya watuhumiwa 65 wa dawa za kulevya.
Hata hivyo, siku chache baadaye, Magufuli alionekana kupinga maelezo ya
Nape kwa kusisitiza kuwa vita dhidi ya dawa za kulevya isiangalie majina
ya watu kwa sababu athari zake ni kubwa kwa taifa.
WALICHOSEMA WABUNGE, WASOMI WANENA
Akizungumzia suala la Mwakyembe, Mbunge wa Kibamba, John Mnyika
(Chadema), alisema ni ishara kuwa baadhi ya mawaziri na viongozi wengine
wamekuwa wakikurupuka kwa kutoa matamko bila kuyafanyia utafiti wa kina
na ndiyo maana Magufuli ametengua agizo alilotoa kuhusu amri ya kuzuia
ndoa kwa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.
Mbunge wa Busega, Dk. Raphael Chegeni (CCM), alisema awali alikuwa
haamini na mwishowe akajikuta akisikitika kusikia tamko la Waziri
Mwakyembe kuhusu zuio la ndoa kwa wasiokuwa na vyeti vya kuzaliwa kwa
sababu agizo lake halikuwa na msingi wa kisheria.
Alisema kupitia mkasa huo wa Mwakyembe, mawaziri wanatakiwa kuwa makini
katika kutoa matamko ya aina hiyo na kwamba, kama wana hoja wanatakiwa
kupeleka ndani ya Bunge ili ijadiliwe.
“Kama unatoa tamko leo na Rais analipinga ama kulifuta, hiyo inaonyesha
kuwa waziri umekurupuka… matamko kama haya yanamgombanisha Rais na
wananchi wake. Mawaziri wajiepusha kutoa matamko ambayo hayajapewa
ridhaa,” alisema Chegeni.
Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), Hussein Bashe, alisema alichokifanya Rais
Magufuli kutengua tamko hilo yupo sahihi kwa kuwa suala la ndoa linagusa
imani ya mtu na serikali haitakiwi kuingilia, na kwamba kama kuna jambo
la kisheria liwasilishwe bungeni ili lifanyiwe kazi.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Richard Mbunda,
alisema inavyoonekana, huenda tangazo alilitoa Mwakyembe ni binafsi kwa
mtazamo wake baada ya kuona kuna udanganyifu mkubwa katika eneo hilo.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Bindamu (LHRC), Dk. Hellen
Kijo-Bisimba alisema agizo la Mwakyembe kuhusu masuala ya ndoa
linashangaza kwa sababu halipo kwa mujibu wa sheria
“Katika Sheria ya Ndoa, vitu ambavyo mtu anatakiwa kuwa navyo ili afunge
ndoa ama sifa, hiyo ya cheti (cha kuzaliwa) haipo… sijui huyo Waziri
ameitoa wapi na pia ingekuwepo kisheria ingepingwa kwa sababu watu wengi
hawana vyeti vya kuzaliwa,” alisema Bisimba.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Ally Bashiru, alisema ni
vyema Rais Magufuli ameingilia na kutengua agizo la Mwakyembe la kuzuia
ndoa kwa asiokuwa na vyeti vya kuzaliwa.