MABAO ya mastraika Mbwana Samatta, Saimon Msuva na Mbaraka Yusuf
waliyofunga wakati Taifa Stars ikizitambia Botswana na Burundi,
imesaidia kuitoa Tanzania shimoni katika orodha ya viwango vya soka vya
Shirikisho la Sola la FIFA.
Katika orodha iliyotolewa jana mchana, Tanzania imechupa kwa nafasi 22
kutoka 157 mpaka 135, ikiwa siku chache tangu nyota hao waliotupia
kambani kuipa Stars ushindi wa mechi mbili mfululizo wa mechi za
kirafiki za kimataifa.
Wakati Tanzania ikipanda kwa nafasi hiyo, majirani wa Kenya wamesogea
kwa nafasi 10 juu kutoka ile ya 88 hadi ya 78 kidunia, matokeo ambayo
yamechangiwa na ushindi kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Congo na sare dhidi ya Uganda.
Uganda wenyewe wamezidi kuonyesha utemi wao kwenye ukanda wa Afrika
Mashariki na Kati baada ya kupanda kwa nafasi mbili kutoka ya 74 hadi ya
72 jambo linalowafanya wawe vinara kwa nchi zilipo kwenye ukanda huu.
Kwa mujibu wa viwango hivyo, Misri inaongoza kwa ubora kwa Afrika ikiwa
nafasi ya 19 kidunia ambapo inafuatiwa na Senegal iliyopo nafasi ya 30
kwa viwango vya FIFA na Cameroon iliyotwaa ubingwa wa Afrika mwaka huu,
ipo nafasi ya 33.
Brazili ndio vinara wa dunia kwa sasa ikiipiku mahasimu wao wa Argentina
walishuka nafasi ya pili, huku Ujerumani ikifuatiwa katika nafasi ya
tatu.