Kuna wakati unaweza ukawa unashangaa kwa nini ndoto zako hazitimii?
Utakuta umejiwekea malengo yako vizuri, lakini unashangaa ni malengo
machache sana yanayotimia au wakati mwingine hakuna kabisa.
Sina shaka yoyote umeshawahi kukutana na hali kama hii wakati fulani
katika maisha yako. Kiuhalisia, yapo mambo mawili ambayo kitaalamu
hupelekea ndoto zako kushindwa kutimia ikiwa hutayajua vizuri.
Jambo la kwanza, ni kutokujua kile unachokitaka vizuri. Hili ni jambo
ambalo hupelekea wengi kushindwa kufanikisha ndoto zao kabisa. Kama
hujui kile unachokitaka vizuri, suala la kufanikisha ndoto zako litakuwa
gumu kidogo.
Katika akili yako ili uweze kufanikisha ndoto yako au jambo unalolitaka
kwa urahisi, ni lazima kile kitu unachokitaka uweze kukijua vizuri.
Tambua njia utakazotumia hadi kukipata kitu hicho pia tambua kitu hicho
changamoto zake ni zipi.
Acha kufanya kosa la kuuchanganya ubongo wako kwa kuupa vitu vingi. Kuwa
maalumu kwa kujua vizuri kile unachokitaka. Usipojua kile unachokitaka
kwa uhakika na kukifanyia kazi, ni wazi hutaweza kufanikiwa na hilo
halina ubishi.
Jambo la pili, ni kukosa hamasa ya kutosha kwa kitu hicho unachokitaka.
Hamasa ni kitu cha muhimu sana ili kufikia ndoto zako. Ukishakijua kitu
hicho vizuri, hamasa itakusaidia kufanya kila jitihada hata kama
umechoka.
Wengi ni watu wa kutaka kufikia lengo fulani katika maisha yao, lakini
kwa bahati mbaya hujikuta ni watu wa kukosa hamasa ya kuwasukuma kuweza
kukamilisha malengo yao.
Ili kufanikiwa, fanya kila ufanyalo kuhakikisha una hamasa ya kufanya
hicho unachotaka kukifanya katika maisha yako. Inapotokea hamasa hiyo
umeikosa acha kusimama eti kwa sababu ya kukosa hamasa.
Maisha hayasimami eti kwa sababu wewe hujisikii kufanya kitu fulani au
umekosa hamasa. Endelea kusonga mbele, huku ukitafuta hamasa ya
kufanikiwa kwako kila siku. Ukifanya hivyo utafika mbali kimafanikio.
Katika hali ya kawaida, kama kila wakati unakosa mambo haya mawili suala
la kufanikiwa kwako linakuwa ni gumu sana. Hivyo, ni lazima sana kwako
kujua vizuri kile unachokitaka na kuwa na hamasa kubwa yaani ‘burning
desire’ ya kuhakikisha kitu hicho ni lazima unaweza kukipata.
Ukichunguza watu wengi ambao hawajafanikiwa wanashindwa kufanikiwa kwa
sababu hizi mbili tu na si vinginevyo. Kama unafikiri natania anza
kufatilia, huku lakini ukianza na wewe.
Kama unajiona hujafanikiwa vya kutosha jiulize binafsi je, unakijua
vizuri kile unachokitaka na huna tamaa ya kutaka hiki mara kile na
mwisho wa siku kuwa na malengo mengi yasiyotekelezwa?
Usiishie hapo tu, tena kama unaona hujafanikiwa vya kutosha jiulize, je,
una hamasa kubwa ya kuona ndoto zako zinatumia? Je, unakosa usingizi na
kuamua kujituma usiku na mchana hadi kufanikiwa?
Ukipata majibu ya maswali hayo yatakusaidia sana kuweza kufanikiwa na
kuwa mtu mwingine tofauti na hatimaye kuweza kufanikisha zoezi zima la
kutimiza ndoto zako. Jitoe kikamilifu kuona ndoto zako zinatimia kwa
kuyajua mambo hayo mawili.
Ni wako rafiki katika mafanikio,