Kwa siku za hivi karibuni wakazi wanaoishi pembezoni mwa Barabara ya
Morogoro katika maeneo ya Kimara na Mbezi jijini Dar es Salaam
wamekumbwa na vilio mbalimbali kufuatia nyumba zao kuvunjwa kwa kujenga
katika hifadhi ya barabara kitendo ambacho ni kinyume na sheria.
Baadhi ya wakazi hao ambao nyumba zao zina alama ya X wameamua kubomoa
wenyewe ili kuepuka kuharibu na kupoteza mali zao wakati Wakala wa
Barabara (TANROADS) atakapoendesha zoezi la ubomoaji nyumba hizo. Lakini
wengine kutokana na mateso waliyopitia kuweza kujenga makazi yao,
hawana ujasiri wa kuyabomoa wenyewe na hivyo kuishia kuangua kilio
wakati yakibomolewa na serikali, huku wengi wakisikika wakisema, hawana
pakwenda.
Zoezi hilo la kubomoa nyumba zilizopo katika hifadhi ya barabara,
halikumuacha salama Mbunge wa Mikumi kwa tiketi ya CHADEMA, Joseph Haule
maarufu Profesa Jay kwani naye nyumba yake ya kifahari ambayo ipo eneo
la Mbezi Luis imewekewa alama ikiashiria kwamba inatakiwa kubomolewa.
Muonekano wa nje wa nyumba ya Mbunge wa Mikumi, Joseph Haule.
Nyumba ya kifahari ya Profesa Jay si pekee itakayobomolewa kwani kuna
nyumba nyingine ambazo zipo ndani ya mita 60 ambalo ni eneo la hifadhi
ya barabara zitakazobomolewa na nyingine tayari zimebomolewa.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) tayari limekata umeme kwenye baadhi
ya nyumba zitakazobomolewa ili kupisha majanga wakati wa zoezi la
ubomoaji.
Wananchi wa meneo hayo wameitaka serikali kuzungumza nao kabla ya
kuendesha zoezi hilo la ubomoaji kwani wamejenga nyumba hizo kwa
kujikongoja sana hivyo kuzibomoa kwa siku moja inawatia uchungu sana.
7 Aug 2017
New