Katika umri wa miaka 24, Ulimwengu anakwenda wapi baada ya kuondoka Sweden? - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Dec 2017

Katika umri wa miaka 24, Ulimwengu anakwenda wapi baada ya kuondoka Sweden?

JUNI 14, 1993 ndiyo alizaliwa Thomas Ulimwengu mahala mkoani Dodoma. Miaka 14 baadaye alikuwa sehemu ya wachezaji vijana U17 ambao walijumuhishwa katika kikosi cha timu ya soka ya mkoa huo kilichocheza michuano ya kwanza ya vijana Copa Coca Cola.


Akicheza eneo la mashambulizi Tom hakuishia katika michuano hiyo tu iliyofanyika Dar es Salaam bali uwezo wake ulimpatia nafasi ya kuchaguliwa na kuendelezwa katika kituo cha soka TSA kilichokuwa chini ya Shirikisho la Soka nchini-TFF.

WAKATI TIMU YA Taifa ya Tanzania Bara U17 ilipomaliza katika nafasi ya pili katika michuano ya vijana ya Cecafa mwaka 2009, Tom aliweza kutengeneza imani kubwa kwa wadau wa soka nchini baada ya kutwaa tuzo ya mfungaji bora wa michuano hiyo iliyofanyika nchini Burundi.

Klabu ya Moro United ilimsaini kwa makubaliano maalumu ya TSA kijana huyo kwa ajili ya kumtumia katika ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2009/10. Kutokana na tamaa ya kutaka kufanikiwa haraka kimpira na majukumu mbalimbali ya timu za Taifa za vijana, Tom alishindwa kutulia Moro United.

Mwaka 2010 alifunga magoli kumi na kushinda tuzo nyingine ya ufungaji bora wakati alipokuwa akiiwakilisha timu ya Taifa U17 katika michuano ya Copa Coca Cola Afrika-michuano ambayo ilifanyika nchini Afrika Kusini.

Baada ya kuonyesha kiwango kizuri katika michuano ya Copa Coca Cola Afrika, Julai, 2010, Tom aliweza kufanikiwa kujiunga na Athletic Football Club (AFC) ya Sweden wakati huo akiwa na miaka 17. Wakati yupo AFC alipata nafasi ya kwenda kufanya majaribio katika klabu ya Humberg ya Ujermani, lakini Julai 2011 alijunga na TP Mazembe ya DR Congo.

Misimu mitano TP Mazembe

Kujiunga Mazembe iliyokuwa bingwa wa Afrika mwaka mmoja nyuma huku pia kukiwepo na wachezaji wa kiwango cha juu kama Tresor Mputu na rafiki yake Mbwana Samatta ambaye pia alikuwa amejiunga na klabu hiyo bingwa mara tano ya Afrika akitokea Simba hakukumuogopesha Tom na badala yake kulimuongezea hamasa ya kufanya kazi yake kwa nguvu akiamini anaweza kutumia klabu hiyo kubwa Afrika kufika mbali kimpira.

Tom kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa kiafrika wana ndoto za kucheza katika ligi kubwa za Ulaya. Alishinda mataji matatu ya ligi kuu DR Congo, taji moja la Afrika na hadi anaondoka klabuni hapo mwaka mmoja uliopita mchezaji huyo alikuwa sehemu ya mipango ya klabu na mmiliki wake Moise Katumbi.

Juni mwaka uliopita Tom alikuwa ni sehemu ya kikosi cha TP ambacho kiliichapa Yanga katika mchezo wa hatua ya makundi katika Caf Confederation Cup. Tom alicheza kwa kiwango cha juu mno katika mchezo huo ambao Yanga ilipoteza 1-0, lakini mwezi mmoja baadae mchezaji huyo akatangaza kutosaini mkataba mpya ambao TP walikuwa wamempa.

Sababu kubwa iliyotajwa wakati huo ni kuwepo kwa ofa nyingi huku meneja wa mchezaji huyo akinukuliwa mara kadhaa kuwa ‘zilifika ofa zaidi ya kumi’ kutoka Ulaya na klabu nyingine kubwa za Afrika. Wengi tulisubiri kuona kama ni kweli Besiktas ya Uturuki watamsaini mchezaji huyo, Rennes ya Ufaransa, Standard Liege, Oostende za Ubelgiji ama Esperance na klabu nyingine ambazo zilikuwa zikitajwa kumtaka.

Kuna baadhi ya wadau wa soka walikubaliana haraka na umamuzi wa Tom kuachana na Mazembe huku wakitoa sababu kuwa mmiliki wa klabu hiyo ni mgumu mno kuuza wachezaji wake hata barani Ulaya. Kutajwa mara kwa mara kwa klabu maarufu za Afrika na Ulaya kuwa zinamuhitaji Tom ndio kulipekea washauri wake kumzuia kusaini mkataba mwingine Mazembe jambo ambalo nililipinga sana wakati ule.

Ni ngumu sana mchezaji asiye na timu kupata klabu nzuri barani Ulaya na kitendo cha kukaa nje ya uwanja kati ya Septemba hadi Januari kulimpoteza zaidi mchezaji huyo na kushusha thamani yake haraka. Alikuwa na nafasi ya kushinda Caf Confederation Cup 2016 kwani baada ya kumalizika kwa mkataba wake na kugoma kusaini mwingine klabu hiyo ilikwenda kushinda taji la kwanza la michuano hiyo. Ambalo pia wamefanikiwa kulitetea msimu huu.

Alitoka klabu kubwa na kujiunga klabu ndogo

Achana na majeraha yanayomuandama mara kwa mara katika mwaka wake mmoja AFC Eskilstuna ya Sweden kwani hata wakati yupo TP Mazembe, Tom alikuwa mchezaji asiyeishiwa majeraha ya mara kwa mara. Kitendo cha kukubali kujiunga na AFC Eskilstuna upande wangu sikukipenda hasa kwa kiwango cha mchezaji huyo kilivyokuwa.

Tom tayari alikuwa mchezaji muhimu wa klabu kubwa Afrika ambako alidumu kwa misimu mitano. Ilishangaza sana wakati niliposikia amerejea AFC mahala ambako alianzia soka la kulipwa akiwa U17 mwaka 2010. Tom alirejea katika klabu hiyo kwa vile alikosa ofa mahala kwingine. Na hilo linatokana na uwepo wa ‘watu wengi’ wa kati na si mawakala ambao huzungumza na klabu zinazohitaji wachezaji.

Kujiunga AFC ilikuwa ni sawa na kurudi hatua nyingi nyuma katika jitihada ambazo alizifanya kwa miaka sita kucheza soka la kulipwa na lenye mafanikio. Katika umri wake wa miaka 24 hivi sasa, Tom anaweza kuibuka tena na kuwa mchezaji  mkali lakini lazima akubali kuwa alifanya kosa kuachana na klabu kubwa na kujiunga klabu ndogo, labda kwa vile Mazembe iko Afrika na AFC iko Ulaya.

Anaondoka AFC anakwenda wapi?

Tayari nimemsikia meneja wake Jamal Kisongo kuwa Tom anaondoka AFC, tena anaondoka kwa makubaliano ya kuvunja mkataba wake uliobakiza msimu mmoja katika klabu hiyo iliyoshuka daraja na kurejea katika ligi ya chini.

Katika maelezo aliyonukuliwa Kisongo anasema Tom anasubiri wakati wa usajili wa dirisha dogo ufike ili asajili katika klabu mpya. Najiuliza inawezekana vipi mchezaji huyo akapata usajili wakati kwa msimu mzima aliokuwa AFC hakucheza kutokana na majeraha? Nahitaji kumuona Tom akicheza katika klabu ya hadhi yake popote pale, ila ni wapi ataenda sasa? Hilo ni jibu ambalo tutalipata wakati utakapofika.