Lukuvi Amaliza Mgogoro wa Muda Mrefu Vingunguti Ataka Kampuni ya PPM Kurejesha Nyaraka za Wananchi - MULO ENTERTAINER

Latest

22 Dec 2017

Lukuvi Amaliza Mgogoro wa Muda Mrefu Vingunguti Ataka Kampuni ya PPM Kurejesha Nyaraka za Wananchi


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi ameumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya wakazi wa Mtaa wa Mtambani Vingunguti na mwekezaji kampuni ya PPM.

Waziri Lukuvi amesema Serikali haitambui uwekezaji uliokuwa ufanyike na kwamba, mwekezaji hakufuata utaratibu hivyo kusababisha mgogoro huo.

Eneo hilo la eka 228 lina jumla ya nyumba 4,000 na wakazi 70,000.

"Hatuzuii mtu kuuza mali yake, tunachosimamia haki itendeke na utaratibu ufuatwe lakini katika mchakato huu mambo yamekwenda ndivyo sivyo," amesema Lukuvi leo Alhamisi Desemba 21,2017.

Amesema, "Kuanzia leo nasema haya maeneo ni mali ya wananchi kama anataka kununua aanze upya kufuata utaratibu uliowekwa, haiwezekani mtu anakuja kuwanunua watu 70,000 kienyeji."

Inadaiwa mwekezaji huyo alitaka kununua eneo hilo kwa ajili ya kujenga bandari kavu.

Kwa mujibu wa wananchi wa eneo hilo tangu mwaka 2012 mwekezaji huyo aliwazuia kufanya shughuli zozote za uendelezaji kwa kile alichodai ameshafanya tathmini.

Hata hivyo, hadi sasa hakuna kinachoendelea na malipo hayajafanyika.

Alipoulizwa kinachoendelea katika uwekezaji huo, meneja mradi wa PPM, Deogratius Chacha amesema wapo katika hatua za mwisho na malipo yangefanyika ndani ya siku 90.

Wakazi wa eneo hilo wamemwambia waziri Lukuvi kuwa mwekezaji amechukua pia leseni zao za makazi na picha.

Kauli hiyo imemfanya waziri Lukuvi kutoa agizo kwa meneja huyo kuwarudishia nyaraka wakazi wote hadi ifikapo kesho saa tano asubuhi.

"OCD chukua vielelezo vya meneja, hakikisha hadi kufikia kesho saa tano awe amewarudishia wananchi nyaraka zao, kinyume cha hapo mkamate mweke ndani," amesema.