Wanaharakati wa Haki za Binadamu Wakosoa Hatua ya Bunge Kuondoa Ukomo wa Umri wa Urais - MULO ENTERTAINER

Latest

22 Dec 2017

Wanaharakati wa Haki za Binadamu Wakosoa Hatua ya Bunge Kuondoa Ukomo wa Umri wa Urais

Wanaharakati wa haki za binadamu wamekosoa hatua ya Bunge kuifanyia marekebisho Katiba ili kumwezesha kiongozi wa nchi hiyo mwenye miaka 73, Yoweri Museveni kurefusha muda wa uongozi.

Wanaharakati wamesema hatua hiyo inarudisha nyuma demokrasia na uamuzi wa wananchi.

Hata hivyo, msemaji wa chama tawala cha NRM, Rogers Mulindwa amekanusha madai kuwa kubadilishwa kipengele cha umri kwenye Katiba kulilenga kumnufaisha Rais Museveni.

Kipengele cha Katiba ya sasa kinaweka ukomo wa umri wa mgombea urais kuwa miaka 75, hali ambayo ingemzuia Museveni kugombea katika uchaguzi ujao wa mwaka 2021 kwa muhula wa sita.



Wanaharakati wa Haki za Binadamu Wamekosoa Hatua ya Bunge Kuondoa Ukomo wa Umri wa Urais
Wabunge 315 walipiga kura kuunga mkono marekebisho hayo, huku 62 wakiyapinga. Wabunge wa chama tawala waliopiga kura ya Hapana walizomewa na wenzao.

Awali, kulizuka mvutano katika jengo la Bunge, wakati baadhi ya wabunge walipokabiliana na watu wa usalama ambao waliwazuia kuingia bungeni ambako kulikuwa kukiendelea mjadala.

Wabunge pia wamerejesha ukomo wa vipindi viwili vya kuwa madarakani kutoka miaka saba hadi miaka mitano, hivyo wabunge wa sasa wataendelea kuongoza hadi mwaka 2023.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya siku tatu za wabunge kujadiliana, huku kukishuhudiwa ulinzi mkali ndani na nje ya Bunge ambapo wakati fulani hata wabunge wenyewe walivutana mashati.

Muswada wa sasa utakuwa sheria baada ya Rais Museveni kuutia saini.

Muswada mpya pia umerejesha ukomo wa mihula ya Rais kuwa madarakani, sheria ambayo iliondolewa ilipofanyiwa marekebisho wakati wa kuingizwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 2005.

Hii inamaanisha kuwa katika uchaguzi ujao Rais Museveni ataweza kuwania urais kwa mihula miwili ambapo akichaguliwa atakaa madarakani mpaka mwaka 2031.