Mbunge Kuanzisha Darasa la Viazi Lishe - MULO ENTERTAINER

Latest

17 Dec 2017

Mbunge Kuanzisha Darasa la Viazi Lishe

 Ili kukabiliana na changamoto ya utapiamlo na lishe duni wananchi wametakiwa kuweka nguvu katika kilimo cha viazi lishe.

Takwimu zinaonyesha tatizo la lishe duni ni changamoto nchini na asilimia 30 ya Watanzania wakiwemo watoto wanakumbana na tatizo hilo.

Mbunge wa Mkinga, Dunstan Kitandula amesema hayo leo Jumamosi Desemba 16,2017 akipokea mbegu za viazi lishe kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo ya Ukiriguru.

Kitandula ambaye pia ni mwenyekiti wa wabunge wahamasishaji wa masuala ya lishe amesema amechukua mbegu hizo kwa ajili ya kuanzisha shamba darasa jimboni kwake atakalolitumia kuwafundisha wananchi umuhimu na namna ya kulima zao hilo.

Amesema ni ajabu kuoana ukosefu wa lishe unaendelea kuwasumbua watoto wakati viazi lishe vinaweza kutumika kama dawa ya kukabiliana na hali hiyo.

“Serikali inajitahidi kukabiliana na changamoto hii lakini naona bado na sisi kama wabunge tuna jukumu la kuingilia kati na kutoa elimu kwa wananchi,” amesema.

Mbunge Kuanzisha Darasa la Viazi Lishe
Amesema wamezungumza na jukwaa la wadau wa kilimo (Ansaf) ambalo limekubali kuwezesha upatikanaji wa mbegu na wabunge watakwenda kupanda katika majimbo yao ili kusambaza elimu.

Kitandula ni miongoni mwa wabunge waliowezeshwa kupata mbegu na Ansaf. Mwingine ni Mbunge wa Urambo, Margaret Sitta.

“Hakuna sababu ya kuendelea kuwa na watu wenye utapiamlo, tutahamasisha viazi hivi vilimwe hata shuleni ili changamoto ya chakula kwa wanafunzi itatuliwe,” amesema.

Amesema eka moja ya viazi lishe ina uwezo wa kumpatia mkulima kati ya Sh15 milioni na Sh20 milioni.

Mtafiti kutoka taasisi ya Ukiriguru, Erick Chang’a amesema tafiti za kisayansi zinaendelea na zimepatikana mbegu bora za viazi lishe zinazostahimili magonjwa.

Amezitaja aina ya mbegu za viazi lishe ambazo zimeonekana kuwa na matokeo bora zaidi ni kabode, kakamega na mataya.

Amesema, “Licha ya kuwa vinaingiza fedha kwa wale wanaofanya kilimo cha biashara viazi lishe ni vizuri kwa wajawazito na ni chanzo kikubwa cha vitamini A ambayo inasaidia uwezo wa macho kuona na kuifanya ngozi kuwa nzuri.”