Nauli Mabasi ya Mkoani Pasua Kichwa Yapandishwa Kinyemela - MULO ENTERTAINER

Latest

16 Dec 2017

Nauli Mabasi ya Mkoani Pasua Kichwa Yapandishwa Kinyemela

Nauli Mabasi ya Mkoani Pasua Kichwa Yapandishwa Kinyemela
Nauli za mabasi yaendayo mikoani katika stendi kuu ya Ubungo zimebainika kupandishwa kinyemela tofauti na bei elekezi iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra).

Mwenyekiti wa bodi ya Sumatra Dk John Ndunguru jana alitembelea stendi hiyo na kukagua namna abiria wanavyohudumiwa hasa kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Katika ukaguzi uliofanyika, baadhi ya mabasi yamekamatwa likiwamo linalofanya safari za Dar es salaam na Arusha kwa kuongeza nauli kinyume na ilivyopangwa na Sumatra.

Dk Ndunguru alisema changamoto ni nyingi hasa magari ya kanda ya ziwa yamekuwa yakichezewa vidhibiti mwendo vilivyofungwa.

“Changamoto ipo kwa magari ya kaskazini mtu anayekwenda Same, Mwanga na Moshi nauli yake ni Sh22,500 lakini wapo wanaotozwa Sh35,000. Nawaagiza makamanda kuwafuatilia wote na kuwafikisha kituoni,” alisema Dk Ndunguru.

Dereva wa basi la Saratoga linalofanya safari zake Dar es salaam na Mwanza ameilalamikia Sumatra akisema kuna mabasi mengine yanayotoa huduma lakini hayajafungwa vidhibiti mwendo jambo ambalo si sawa.

Beatrice Pendaeli abiria anayesafiri kuelekea Arusha amewataka Sumatra wawe wanafanya ukaguzi wasingoje siku za sikukuu pamoja na kuwachunguza wanaokata tiketi ili kudhibiti feki.

Kamanda wa Polisi kikosi cha usalama barabarani mkoa wa Kinondoni, Saimon Mwangamilo alisema kwa kipindi hiki cha mwisho wa mwaka watu wengi wanakwenda mapumziko huku baadhi ya mawakala wakipandisha nauli kinyemela.

“Jeshi la polisi tumejipanga vizuri, tutahakikisha kipindi hiki cha sikukuu za mwisho wa mwaka tunawakamata mawakala wote watakaopandisha nauli pamoja na kuwafikisha mahakamani,” alisema Mwangamilo.

Pia, aliwashauri wasafiri kukata tiketi kwenye vituo vya mabasi husika badala ya kuwatumia wapigadebe ambao wanapandisha nauli na wengine wanatumia vitabu feki vya tiketi.