Flyover ya Tazara Yawapagawisha Madereva - MULO ENTERTAINER

Latest

19 Sept 2018

Flyover ya Tazara Yawapagawisha Madereva

Flyover ya Tazara Yawapagawisha Madereva
Kero mpya imeibuka kwa abiria wa daladala eneo la Tazara jijini Dar es Salaam baada ya madereva wa daladala za Mnazi Mmoja- Gongo la Mboto kupitiliza vituo wakitumia zaidi barabara ya juu na kuwaacha abiria waliopo vituoni chini.

Hali hiyo imejitokeza leo(jana) ikiwa ni siku nne tangu kuanza kutumika kwa barabara hiyo ya juu (flyover) iliyopo makutano ya barabara za Nyerere na Mandela (Tazara).

Baadhi ya abiria waliozungumza na Mwananchi walilalamika kuwa kwa sasa wanasubiri zaidi ya dakika 10 hadi 60 kabla ya kupata daladala ya Gongo la Mboto- Mnazi Mmoja inayopita barabara ya chini.

Aprili 16, 2016 Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa barabara hiyo, ambapo Agosti 29 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitembelea kukagua  ujenzi huo na kueleza ume kwa asilimia 98 na kwamba ufunguzi utafanyika mwezi ujao.

“Nimeshuhudia jana (juzi) na leo (jana), yaani ili upate kwa haraka daladala ya kwenda Mnazi Mmoja inakubidi kusubiri kituo cha mbele kiitwacho Mtava badala ya kituo cha Tazara kwa sababu (Tazara) kipo chini ya flyover.”

“Daladala wanapitiliza hadi vituo vya mbele na umbali wa kituo hadi kituo ni zaidi ya mita 200 kutembea, kwa hiyo abiria wa kituo hiki tunateseka sana,” alisema Abdul Waisa mmoja wa abiria wanaotumia kituo cha Tazara. 

Baadhi ya madereva wa daladala wamekiri kukwepa barabara ya chini wakidai changamoto hiyo inatokea zaidi wakati wa asubuhi na jioni daladala zinapokuwa zimejaza abiria kutoka katika vituo vikuu.

 “Kabla ya kituo lazima niulize abiria kama atashuka, kama hakuna abiria anayeshuka Tazara hakuna sababu ya kupita barabara ya chini, inanirahisishia kupita juu moja kwa moja hadi kituo cha Mtava na flyover inakuwa imeniondolea muda wa kukaa foleni kwenye round about (makutano),”alisema Said Mohamed kondakta wa daladala za G/Mboto-Mnazi Mmoja.

Kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), kukamilika kwa mradi huo kutapunguza muda wa kukaa kwenye foleni kwa asilima 80, ikimaanisha kutoka wastani wa dakika 45 hadi dakika 10 kuvuka kwenye makutano hayo.