Huyu Hapa Muuza Madawa ya Kulevya Aliyependwa na Wananchi Mpaka Kupewa Jina la Yesu na Mlinzi wa Amani - MULO ENTERTAINER

Latest

18 Sept 2018

Huyu Hapa Muuza Madawa ya Kulevya Aliyependwa na Wananchi Mpaka Kupewa Jina la Yesu na Mlinzi wa Amani



TAJIRI WA UNGA AKAWA MWEMA MPAKA AKAITWA YESU

Christopher Coke a.k.a Dudus, ni tajiri wa dawa za kulevya, akiongoza genge la Shower Posse.

Genge hilo na mtandao mzima wa unga, Dudus au President alirithi kutoka kwa baba yake, Lester Coke a.k.a Jim Brown au Ba-Bye aliyeuawa gerezani mwaka 1992.

Shower Posse makao makuu yake yapo Tivoli Gardens, Kingston, Jamaica.

Dudu alikuwa mtu mwema. Alisaidia fedha familia maskini, alilipia ada wanafunzi ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo, zaidi alitengeneza ajira nyingi kwa vijana.

Hayo yalisababisha apendwe sana. Dudus aliitwa Rais wa Tivoli Gardens, alilindwa na kila mwananchi. Serikali ya Jamaica pia ilimlinda, maana alikuwa mfadhili wa viongozi.

Marekani ilitaka Dudus akamatwe lakini Serikali ya Jamaica haikutekeleza.

Dudus alipokamatwa na Marekani mwaka 2010, kwananchi wa Jamaica, hususan wakazi wa Tivoli Gardens, waliingia mitaani na kuandamana, wakitaka Dudus aachiwe huru.

Wananchi walikuwa na mabango yaliyoandikwa kuwa Dudus ni mlinzi wa amani ndani ya Tivoli Gardens, hivyo aachiwe. Wapo waliokwenda mbali zaidi na kuandika kwamba kumkamata Dudus ni sawa na alivyokamatwa Yesu kwa sababu ni mtu safi.

Wananchi wa Jamaica, hasa wa wakazi wa Tivoli Gardens, walikuwa hawaambiwi kitu kuhusu Dudus. Tuhuma zote za kuhusika na dawa za kulevya, waliona ni uzushi.

Ijumaa ya Juni 15, 2012, Mahakama ya Kuu ya New York, ilimhukumu Dudus kifungo cha miaka 23 jela. Miaka 20 ikiwa kwa kosa la kupanga njama na kufanya biashara haramu na miaka mitatu kwa kosa la kuuza bunduki Marekani bila utaratibu.

Sheria ya Marekani ni kufilisi mali zote za wauza dawa za kulevya pindi wanapokutwa na hatia, lakini imekuwa vigumu kumfilisi Dudus, maana uwekezaji wake wote ameufanya Jamaica ambako Serikali inamlinda.

Hata sasa, genge la Shower Posse linaendelea na kazi ya usafirishaji wa bangi, cocaine na silaha kwenda Marekani, japokuwa bosi wao yupo jela.

Ipo hofu kuwa hata baada ya Dudus kumaliza kifungo jela, huenda Serikali ya Marekani isimwachie huru kwa sababu ya hofu kwamba atarudi kazini kwake na kuzidi kuwaangamiza Wamarekani kwa kuwauzia dawa za kulevya na silaha haramu.

Huyo ndiye Dudus wa Tivoli
By @luqmanmaloto