Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Humphrey Polepole amesema mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda hakupaswa kufanya sherehe na Polisi kwa sababu kuna mahali hali haikuwa shwari na wao walikaa kimya.
Polepole ameyasema hayo leo Septemba 18,2018 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi ndogo ya CCM Lumumba jijini Dar es salaam akielezea sababu za ushindi wa majimbo mawili ya Monduli na Ukonga.
Amesema Chadema wanasema Jeshi la Polisi linawasaidia CCM ilihali aliyekuwa mgombea ubunge wa chama chao kwenye Jimbo la Ukonga Asia Msangi alimkwida msimamizi wa uchaguzi mbele ya Polisi na walikuwa wametulia.
"Makonda hakupaswa kufanya sherehe nao kwa sababu kuna mahali sheria ya tume ilikuwa inakiukwa na wao wapo wametulia" amesema Polepole.
Amesema pamoja na yote CCM inathamini uwepo wa vyama vya upinzani na wanataka wakosolewe na kupewa mawazo mbadala.
"Kwa bahati mbaya hawa wenzetu kazi yao ni kukosoa tu" amesema
Pia, Katibu huyo aliutaka upinzani utambulike kwa itikadi za vyama vyao badala ya kuonekana mtu zaidi ya chama.
"Kama chama kinachojinasibu kuwa ni mpinzanii mkuu na ninachelea kukiita mpinzani na ninashukuru wameshindwa vibaya, ukimtoa yule kiongozi wao na wapambe wake wa karibu Kinabaki nini, ACT Wazalendo ukimtoa mjomba kinabaki nini.”
"Wajenge kwanza itikadi ya vyama vyao itambulike, CCM ni taasisi inayotambulika kiitikadi" amejinasibu Polepole.