JINSI YA KUIPATA AMANI YA MOYO PENZINI! - MULO ENTERTAINER

Latest

13 Sept 2018

JINSI YA KUIPATA AMANI YA MOYO PENZINI!

UKIFANYA utafiti kwa vijana wengi kwa sasa kuhusu suala la amani ya moyo katika uhusiano wao, asilimia kubwa watakuambia hawana amani. Watu wengi wanalia kwenye mapenzi, huyu analia na hili yule analia kwa lingine.  

Kila mmoja ana historia ya chanagamoto yake katika mapenzi. Bahati mbaya sana, mapenzi hayana ‘fomula’ kwamba fulani alipitia njia hii na wewe labda unaweza kuipita ili uwe salama. Kila mmoja anapaswa kujua njia za kupita ili awe salama.

Ili muishi vizuri na mwenza wako, mnahitaji kusomana tabia, kushibana, kuvumiliana na kutengeneza njia zenu za kupita ambazo hazitakuwa na madhara kwa pande zote. Kabla ya kutengeneza njia yenu, hakikisha tu kwamba una mtu sahihi ambaye ana sifa ambazo unazitaka au zinazopaswa kuwa kwa mwanaume au mwanamke anayejiheshimu.

Baada ya kuona ana sifa, anzeni safari ya urafiki na uchumba na hapo ndipo kwenye changamoto. Ni wakati ambao kila mmoja anakuwa anamsoma mwenzake tabia hivyo uvumilivu na busara zaidi katika kufanya uamuzi.

Vijana wengi wakiwa kwenye hatua hii ndipo wanapokutana na visa mbalimbali ambavyo vinawatoa kwenye mstari na kujikuta wakishindwa kufanya uamuzi sahihi. Mwanaume anaumia moyoni pale mwanamke aliyemuamini, aliyemkabidhi moyo wake anapogeuka pasua kichwa kutokana na hulka au tabia fulani.

Vivyo hivyo kwa mwanamke, yawezekana mwanaume ambaye anamhitaji, anamuamini akampa mateso makali ya kitabia ambayo yanamfanya hata ajute kuwa naye. Bahati mbaya sana hata akisema aachane na mtu huyo, anaambulia maumivu makali maana anakuwa ni mtu ambaye amemzoea.

Anaumia sababu alikuwa anatamani waweze kufika mbali katika safari yao hivyo anakosa jinsi ya kufanya maana anakuwa ameshafanya kila jitihada kumuweka sawa mwenzake, lakini inashindikana. Hicho ndicho kipindi cha kuchanganyikiwa. Kipindi cha kuyumba hata katika mambo ya kawaida ya kiutendaji wa maisha kwa jumla.

Mtu unashindwa kufanya kazi zako kwa ufanisi kwa sababu ya kuvurugwa. Kama ni bosi kazini, unakuwa mkorofi. Kama ni mfanyakazi wa kawaida unakuwa na majibu ya ajabu kwa wafanyakazi wenzako. Kama ni mfanyabiashara, mambo yanakwenda ndivyo sivyo. Jamani pamoja na kuwepo kwa mapenzi, itafute sana amani ya moyo.

Dhibiti hisia zako, sema na moyo wako. Kataa kuharibu mambo kwa sababu tu ya mapenzi. Akili yako ina zaidi ya majibu ya changamoto unazokutana nazo. Tumia muda na uwezo wako wote kupigania penzi lako, lakini weka akiba ya moyo wako. Usiutese kiasi cha kushindwa kufanya mambo yake ya msingi.

Tatua changamoto, lakini ukiona ni nzito, kaa pembeni. Jipe muda wa kutafakari upya mwenendo wa uhusiano wako na ukiona haiwezekani, suburi umpate mwingine. Kubali kumuacha aende, kataa kubaki na maumivu muda wote. Jiulize wewe unaumia kwa sababu yake, je, na yeye anaumia kwa sababu yako? Kwa sababu gani uumie na mtu ambaye hana habari na wewe? Mwache aende!

Hakikisha tu unapompata mwingine, usiruhusu moyo wako kuzama kabla ya kujiridhisha kama ni mtu sahihi ndipo umpende zaidi. Maisha mengine mazuri yapo bila yeye. Muombe Mungu akupe mtu sahihi, usahau makovu yote ambayo utakuwa umeyapata!
Tukutane wiki ijayo hapahapa. Unaweza kunifuata kwenye mitandao yangu ya kijamii. Instagram na Facebook natumia Erick Evarist, Twitter natumia ENangale.