Kimbunga Florence Chaanza Kupiga Marekani, Chaofiwa Kikawaua Watu Wengi - MULO ENTERTAINER

Latest

14 Sept 2018

Kimbunga Florence Chaanza Kupiga Marekani, Chaofiwa Kikawaua Watu Wengi

Kimbunga Florence Chaanza Kupiga Marekani, Chaofiwa Kikawaua Watu Wengi
Upepo mkali unaotokana Kimbunga Florence ambacho kinatishia watu wengi Marekani kimeanza kupigia maeneo ya pwani ya mashariki ya Marekani.

Maafisa wameonya kwamba huenda mawimbi makubwa ya kutoka baharini na mvua kubwa vikaathiri maeneo ya North na South Carolina, huku kimbunga hicho kikielekea maeneo ya bara.

Upepo wa kimbunga hicho unavuma kwa kasi ya maili 100 kwa saa (155 km/h).

Nyumba takriban 100,000 tayari hazina huduma ya umeme huku hali ikitarajiwa kuwa mbaya zaidi.

Maafisa wa serikali wametahadharisha kwamba kimbunga hicho kinaweza "kuwaua watu wengi sana" huku kukiwa na wasiwasi wa kutokea mafuriko "mabaya sana".

Watu zaidi ya milioni moja katika maeneo ya pwani North Carolina, South Carolina na Virginia walikuwa wametakiwa kuyahama makazi yao.

Maelfu walitafuta hifadhi katika vituo vya muda vya huduma za dharura Alhamisi usiku.

Hali ilibadilika na kuwa mbaya zaidi Alhamisi huku upepo ukiongeza nguvu kiasi katika maeneo ya pwani.

Katika baadhi ya maeneo ya North Carolina mvua ya kina cha futi moja ilinyesha katika kipindi cha saa kadha, na picha zilionyesha maji yakijaa baharini na kufunika maeneo ya ufukweni.


Sasa Kimbunga Florence ni cha kiwango cha pili na hakujakuwa na dalili zozote za kupunguza nguvu kwenye kitovu chake kabla ya kufika maeneo ya bara Ijumaa asubuhi.

Watabiri wa hali ya hewa wametahadharisha kwamba maji ya mafuriko huenda yakafikia kina cha futi 13 (mita 4) na katika baadhi ya maeneo, huenda upepo mkali ukasababisha maji ya mito kuanza kurudi nyuma.