Ugumu wa Lowassa Kuingia Ikulu Oct 2015 Huu Hapa - MULO ENTERTAINER

Latest

18 Aug 2015

Ugumu wa Lowassa Kuingia Ikulu Oct 2015 Huu Hapa

WAKATI wafuasi wa vyama vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa) wakiwa na shangwe kutokana na kumpata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa kama mgombea wake wa urais katika uchaguzi mkuu wa Oktoba, ugumu wa kiongozi huyo kuingia ikulu umebainishwa, Uwazi lina habari kamili.


aliyekuwa waziri mkuu wa kwanza wa serikali ya awamu ya nne chini ya Rais Jakaya Kikwete, alijiunga na Chadema mwishoni mwa Julai mwaka huu baada ya jina lake kukatwa wakati wa mchakato wa kutafuta mgombea urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), nafasi ambayo ilitua kwa Dk. John Pombe Magufuli.

Ugumu wa kwanza unaotajwa, ni uwezekano wa kutopigiwa kura na wafuasi wote wa Chadema, ambao kuingia kwa kada huyo wa zamani wa CCM, kuliwagawa, kwani wapo waliokubali kwa roho moja ujio wake na wengine ambao hawakupendezwa kabisa na jambo hilo. Mgawanyo huo, unapunguza kura ambazo angeweza kuzipata endapo wanachama hao wangekuwa kitu kimoja kama awali.

Ingawa aliripotiwa kuwa na wafuasi wengi akiwa CCM, ushahidi unaonesha kuwa siyo mashabiki wake wote wamefurahishwa na hatua yake ya kuhamia upinzani, hivyo idadi kubwa ya wapiga kura aliokuwa akiwategemea, wameamua kuachana naye na wao kuendelea kubakia chama tawala.
Ugumu mwingine, unatokana na ukweli kuwa licha ya Chadema kujizatiti hadi vijijini, lakini haina mtandao mpana kama ilivyo kwa CCM, hivyo hata ile ‘amsha amsha’ inayoonekana mijini hivi sasa, haiko vijijini, ambako chama tawala bado kina mizizi na kina wapiga kura wengi maeneo hayo.
Jambo lingine linalotajwa kuwa ni gumu kwa Lowassa kuingia ikulu, ni ukweli kuwa kujiweka kando kwa viongozi wawili waliokuwa na mashabiki wengi, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wa Cuf, Profesa Ibrahim Lipumba kumewachanganya mno wafuasi wao na hivyo kuwa njia panda.

Ukimya wa Dk. Slaa, anayeaminika kufanya kazi kubwa ya kuwashawishi watu kuipenda Chadema, umewafanya baadhi ya wafuasi wake kutokuwa na mwelekeo, hivyo kuweka uwezekano mkubwa wa watu hao ama kupiga kura kwa wagombea wa vyama vingine au wasipige kabisa, kitu kitakachopunguza kwa kiwango kikubwa idadi ya kura za Lowassa kuelekea ikulu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI